Thursday, August 18, 2016

KUMBATO NI TIBA

Kumbato mara nyingi hutumika tunaposalimiana ama kuagana kwa furaha na wapendwa wetu. Hii ni ishara ya furaha na mara nyingi huchukua sekunde chache sana kama 3 mpaka 6. 

Tunaposalimiana kwa mikono tunakuwa na umbali kiasi flani na ndiyo maana tunapokuwa makazini ama tukikutana na watu kwa mara ya kwanza tunapeana mikono kwa kuwa hatujawa karibu kiasi cha kuonyesha hisia zetu hasa za furaha kwao.

Kitendo cha kukumbatia ni sehemu mojawapo ya kudumisha upendo kati yetu na tuwapendao. Na kumbato hilo hilo hugeuka kuwa tiba hasa tunapotumia sekunde nyingi zaidi walau 20 na kuendelea.


Unapomkumbatia mtu ipasavyo, unakuwa na nafasi kubwa sana ya kuondoa ugonjwa, kutuliza hasira, kutuliza au kuondoa shauku, kutoa upweke, kupoteza huzuni na hata kupunguza na kuondoa kabisa msongo wa mawazo.
Tuangalie manufaa ya kumbato kwa undani wake:
  • Malezi yanayohusisha mguso wa kumbato hujenga hali ya uaminifu na hisia ya usalama. Hii husaidia kuleta mawasiliano ya wazi na yenye uaminifu.
  • Kumbato linaweza kuongeza kiwango cha Oxytocin papo hapo na kukuinulia hisia chanya. Nayo hutoa hisia ya upweke, kutengwa, shauku kali na hasira.
  • Kukumbatia kwa muda mrefu hunyanyua viwango vya Serotonin hivyo kuinua mudi ya kujenga furaha.
  • Kumbato huimarisha mfumo wa kinga hivyo kukulinda na magonjwa. Shinikizo la taratibu katika Sternum na chaji za hisia, hujenga na kufanya Solar Plexus Chakra kuwa hai hivyo kuchochea kongosho tezi, ambayo husimamia uzalishwaji wa seli nyeupe za damu mwilini. Solar Plexus Chakra ni msingi wa utu wetu, utambulisho wetu na u-sisi wetu.

  •  Unapokumbatia unalegeza mishipa. Hii huondoa mvutano mwilini mwako na kukuondolea maumivu kwa kuongeza mzunguko katika tishu laini hivyo kukupoza na kukupa tulizo.
  • Kumbato huweka usawa katika mfumo wa neva. Majibu ya mtu ya ngozi ya Galvanic katika kutoa na kupokea kumbato huonyesha mabadiliko ya nguvu katika ngozi. Athari ndani ya unyevu na umeme katika ngozi hupendekeza hali ya usawa zaidi katika mfumo wa neva.
  • Ni jambo linalotufundisha kutoa na kupokea. Ukikumbatiana na mtu au watu unapata thamani ya usawa ya kutoa na kupokea joto kama kutoa na kugawana. Inaelimisha juu ya upendo kwa wote wakumbatianao (wawili, watatu au kundi).
  • Kukumbatiana ni kama tafakari ya undani au kicheko cha furaha ambavyo kufdunza kusahau ama kupotezea yale yanayobugudhi, yanayokwaza au kuumiza na kujikita katika usasa yaani kuishi kwa wakati uliopo. 
  • Kumbato hukufanya ujisikie uko hai. Hukupa mzunguko wa mawazo mbalimbali yaliyo katika maumbo tofauti na kukuunganisha na moyo pamoja na pumzi yako.
  • Kumbato huletea hali ya kujiamini. Hali ambayo imekaa ndani yetu toka udogo wetu ambapo tumekuwa tukikumbatiwa na kubebwa kwa upendo na wapendwa wetu kama ndugu jamaa na marafiki. Hisia hizi zimekuwa ndani yetu kadiri tukuavyo hivyo kutujengea nguvu na uwezo wa kujipenda.
  • Kumbato la nguvu linalogusisha mioyo ya wawili wakumbatianao hufanya upendo kati yao kuwa maradufu hivyo kuweka uzio usioweza kuwatenganisha kirahisi kwani upendo ni dawa ya ajabu. 
  • Kumbato pia huimarisha saikolojia yetu na kuleta maendeleo ya miili yetu kwani hukufanya tulivu na mwenye afya ya roho na mwili pia.
  • Nguvu unayobadilishana na umkumbatiaye huwekezwa katika mahusiano yenu (mama na mwana, baba na mwana, marafiki, kaka na dada, wapenzi na kadhalika). Nguvu hiyo huleta hamasa ya uelewa baina yenu na mwisho kuwafanya mdumu.
  • Pia husaidia kunyoosha misuli ya nyuso, kuondoa mikunjo ya uzee pamoja na kufanya uzee uje taratibu ama kupunguza kasi ya uzee.
Varginia Satir ni mtaalamu anayeheshimika katika mambo ya familia. Yeye aliweza kufanya utafiti mdogo na kujiwekea msemo ambao sote tukiuzingatia tunaweza imarisha afya zetu kwa kiwango fulani. Anasema:

*Tunahitaji kumbato mara 4 kwa siku ili KUISHI
* Tunahitaji kumbato mara 8 ili KUREKEBISHIKA / KUIMARIKA
*Tunahitaji kumbato mara 12 ili KUKUA

Kwa wale wapendanao (wapenzi), kumbato ni chanzo kikubwa cha kuboresha mahusiano yenu  na tafiti nyingi zimeonyesha kuwa, wapenzi wanaokumbatiana sana hudumu kwenye mahusiano yao kwa muda mrefu.

Tibu maumivu yako sasa, tibu upweke na hali zote mbaya unazozipata kwa kupata kumbato. Anza kukumbatia watu zaidi kwa tiba rahisi zaidi.

Friday, July 22, 2016

Msukumo / motisha

Endelea kukimbia hata kama ni wa mwisho katika mashindano. Huwezi jua, yawezekama ukawa bingwa.

Ninawakummbusha ndugu zanguni kutokata tamaa maana muda unaokata tamaa unaweza kuwa ndio muda sahihi kabisa kwa wewe kupata mafanikio/ ukitakacho/ ulichoomba kwa muda mrefu/ kufikia ndoto zako na kadhalika.

Ukihisi kuacha usiache, kazana kwa kuwa umekaribia. Sote ni washindi kwa muda tofauti na kwa namna tofauti.

Thursday, July 21, 2016

Kila lililokamilika huanza kwa uamuzi wa kujaribu.


Msemo wa leo ni wa kutuhamasisha zaidi. Kila lililokamilika huanza kwa uamuzi wa kujaribu.

Chukua mfano huu mdogo. Umekaa kochini ukatamani maji ya kunywa lakini unaona uvivu kunyanyuka, hutapata maji. Kuna watu ndani unashindwa kuwaomba msaada wakuletee, hutapata maji. Umepata ila ni ya moto unahitaji ya baridi na huchukui uamuzi wowote, hutakata kiu yako.

Sasa, unataka kufanikisha mipango yako ambayo pengine hujaanza hata kujipanga, hutaikamilisha. Inatakiwa ifikie wakati ambapo utasimama hata kama umechoka au hujiwezi kufedha au kimwili. Anza safari huku ukiomuomba Mungu, naye atakuimarisha ukiwa njiani na utafika salama.

Fanya maamuzi haraka ya wapi uanze ama wapi upite na sio maamuzi ya kuendelea kusubiri. Bora ujaribu ushindwe kuliko usijaribu kumbe unajikosesha faida. Na ukijaribu ukashindwa usikate tamaa haraka, jaribu tena na tena mpaka utakapoona haiwezekani kabisa; ingawaje hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Utachelewa lakini sio kushindwa.

Kazi kwako...

Wednesday, July 20, 2016

Onyesha heshima hata kwa watu wasiostahili; sio kwa muonekano wa tabia zao ila muonekano wa yako.


Maneno ya Dave Willis yanakumbushia utoaji wa heshima. Waswahili wanasema "heshima ni kitu cha bure" yaani huhitaji kulipia wala kugharamia chochote kuheshimu ama kuheshimiwa ila kujiheshimu na kutoa heshima hiyo kwa wengine wote hata kama hawastahili heshima yako.

Inakuwaje mtu hastahili heshima yako? Ni kwa sababu haonyeshi upendo kwako kama binadamu, sababu anakuona uko chini sana, sababu anakudharau, anakuona hufai kwake na katika maisha yake, sababu huna uwezo kifedha ama kifikra, sababu huwezi kufika alipofika, sababu hujampa alichotaka, hauna muonekano mzuri na mengine mengi.

Zipo sababu nyingi lakini pamoja na yote tunapaswa kukumbuka kuwa sote ni binadamu na tunakosea. Inawezekana tukapishana leo  lakini tukumbuke dunia huzunguka, binadamu pia. Tuheshimiane kwani hatujui ya kesho, inawezekana ukamheshimu mtu leo hata kama hastahili na kesho akawa msaada mkubwa tu kwako. Lakini tukijikweza leo, kesho tutaaibika.

Usimuhemu huyu ukamuacha yule ukidhani unakuwa mwema zaidi. Heshimu wote ili uonekane mwenye heshima.

AFRITRACUL




 Hivi ni vitu vya kiafrika kabisa. Vaa upendeze. Pendeza nasi AFRITRACUL kwa bei nzuri kabisa. Unaweza kutoa oda ya kitu ukitakacho ukatengenezewa. Jumla na reja reja unapata. Karibuni nyote.
























Tuesday, July 12, 2016

AFYA ni nini?


Afya ni hali ya kutokuwa na ugonjwa au kidonda. Afya ni hali ya kuwa na amani ya roho. Afya ni ubora wa akili, mwili na nafsi. Afya hutegemea vitu hivi vitatu kuwa ili kuwa hai na salama:
  • Akili
  • Mwili
  • Nafsi
Akili ni utashi tuliopewa na Mwenyezi Mungu katika kung'amua mambo ulimwenguni. Akili hujumuisha uelewa, ufikiri, uamuzi na utendaji wa mambo. Hakuna awezaye kutafsiri akili yetu ila matendo yetu yanaweza kumfanya mtu aone flani yuko vipi; nayo bado itakuwa mtazamo wake sababu tunatofautiana kufikiri pia. 

Binadamu hutumia akili kila siku na kila wakati ili kuelewa, kufikiri, kuamua na kuhakikisha tunatimiza jambo. Kwa maana hiyo, tunapaswa kuipumzisha "PUMZISHA AKILI". Akili ikichoka mwili nao huchoka na hutafanya chochote sababu haitakuwa na uwezo mzuri kutenda. Lala au oga au ogelea au sikiliza mziki au chochote ukipendacho ambacho hakitakufanya utumie nguvu ya akili.

Mwili ni muundo wote wa binaadam. Ni maumbile ya mtu. Mwili huhusisha yote yaliyotengeneza "mtu" mfano viungo kama miguu, mikono n.k, Maji kama mate, damu n.k, na vingine kama mishipa kucha na nywele.

Tunapaswa kujipenda kwa kula vizuri, kulala vizuri na pazuri, kuvaa vizuri na kujijali muda wote kwa kuuweka mwili salama mfano kwa kupiga mswaki baada ya kula, kuosha nywele mara kwa mara, kukata na kusafisha kucha, kuoga, na kuvaa nguo safi. Pia tujiepushe na hatari, ugomvi na makwazo kwa faida ya mioyo yetu. 

Ukitembea sana juani pata kivuli unywe na maji. Penye baridi uvike mwili wako kwa sweta ama nguo nzito. Ukiumia au kuumwa pata matibabu sahihi kwa kwenda hospitalini. Jipende, Ujali mwili wako. Tukifanya hivyo miili yetu itakuwa salama. 

Nafsi ni roho yenye kuleta imani ndani yetu. Sisi huamini vitu mbali mbali kwa msaada wa nafsi. Lakini yote heri kama tutaamini vitu vyenye kujenga na sio kubomoa. Nafsi pia hutofautiana ya mtu na mwingine ndio maana tukawa tofauti japo chimbuko letu kiuumbaji ni moja. 

Nafsi nayo huhitaji utulivu ili kuupa mwili na akili nguvu za kuishi kwa afya. Pata muda wa kutulia ukiongea na WEWE kujua nini waweza fanya LAKINI, mshirikishe MUUMBA wako kwa yote kupata amani uitakayo moyoni na kwa wakuzungukao.

Hivyo basi, jipe likizo au omba likizo. Tembelea sehemu mbali mbali za starehe au vivutio kutuliza mwili, akili na roho pia. Ongea vizuri na watu, cheka, tabasamu hata kama umeumizwa. Inasaidia sana. 

Afya ya vitu vyote vitatu ni muhimu katika kukuweka mwenye nguvu na furaha.
 Jali afya yako!



Friday, July 8, 2016

KUWA MTU MZURI LAKINI USIPOTEZE MUDA KUTHIBITISHA




Tumeumbwa tupendane lakini haimaanishi umpende kila mmoja sawa sawa. Tunapaswa kusaidiana na kuheshimiana lakini inaposhindikana unaacha. Usiumize kichwa kumfurahisha asiyetaka au asiyestahili. Kakupotezea muache, usimlete karibu kilazima.

Asipokuona mzuri machoni mwake muache sababu wapo wengine maelfu zaidi wanaokuona uko sawa. Hajaona thamani yako muache sababu wapo wengi zaidi wanaotambua uwepo wako na hasa umuhimu wako. 

Timiza wajibu wako kwa kila mmoja katika jamii yako kulingana na nafasi yako kwao. Jali, heshimu, penda, sahihisha, funisha, ongoza, furahisha, onya, lakini kama haionekani kumsaidia unayemfanyia badilisha njia, mtazamo, suluhisho, matendo. Usilazimishe wala kung'ang'ania, utajiumiza.

Yamkini mia wakakusema vibaya, usiumie sababu yupo japo mmoja anayetambua uzuri wako kwa wema wako; na hilo ni kuu mno. Kuwa hivyo ulivyo na uache mengineyo yapite njia yake... 

Monday, July 4, 2016

MAZOEZI SI HAKIKA YA AFYA NJEMA



Mazoezi ni muhimu kwa kukuweka mwenye nguvu muda wote lakini maisha unavyoyaishi pia yanachangia katika kukufanya mwenye furaha, mchangamfu na mwenye afya njema.

Dr. Denis Nturibi anasema kuna vitu vitatu ambavyo binadamu wote tunapaswa kuvifuata ili kuwa na afya njema. Mazoezi ni sahihi kuyafanya lakini muundo wa maisha (lifestyle) yetu unamchango mkubwa pia.

1. Kula sahihi.
Tunapaswa kupata lishe bora kwa maana kwamba tuachane na vyakula ambavyo vinanenepesha hasa vyenye mafuta mengi na sukari nyingi. Tusile sana yaani tule kwa kiwango na kwa muda tu. Kuna watu wanakula kwa siku hata zaidi ya mara nne. Kila unachoona unataka uonje. Basi tujitahidi kujiwekea mipaka yaani nini kiliwe na kwa muda na kiwango gani, Bila kusahau maji ya kunywa (angalau lita moja kwa siku).

2. Pumzika na lala.
Tunafanya kazi kupata hela, sawa kabisa. Hata Mungu anatuambia tufanye kazi na ametuweka duniani hasa kufanya kazi bila hivyo hatupati kula. Lakini kila kitu kiwe kwa kiasi. Pata muda wa kutosha wa kupumzika. Kazi nyingi zinatufanya tutumie akili sana katika kufikiria, kusuluhisha na kudadavua mambo kitu ambacho huchosha sana akili na mwili pia. 
Lala masaa yanayotakiwa (8-10). Usitumie muda mwingi kuangalia luninga ukakesha asubuhi unaelekea darasani au ofisini. Usisome masaa tisa ukalala kwa saa moja au kuvusha kabisa halafu uingie kufanya mtihani. Pumzika  na lala ili akili pia ipumzike na mwili kwa ujumla.

3. Shughuli za kimwili.
Mazoezi ya viungo ni muhimu katika kukufanya mwepesi. Kimbia taratibu (jogging) au tembea kwa mwendo wa haraka kwa umbali kidogo kila siku au walau mara mbili kwa wiki. Hii itakusaidia kukupa pumzi nzuri. Kwa wale waimbaji, sauti yako itapunguza kuhema hema.


Kwahiyo, Dr. Dennis anaeleza vizuri kuwa, mazoezi pekee si afya, lishe na kupumzika pamoja na kulala vinasaidia kwa afya bora.

Unaweza kuwa na mwili mdogo na wenye nguvu sababu ya mazoezi lakini kama unakunywa pombe sana au unavuta sigara utakuwa na nguvu bila afya njema.

Jitengenezee mazingira mzuri ya kuwa na afya muda wote kwani afya njema ndio kila kitu.




Unaweza kushindwa kudhibiti tabia hasi za mtu. Lakini unaweza kudhibiti muda gani unashiriki ndani yake.


Toka upate ufahamu wa kunyambua mambo, leo hii jiulize umeachana na wangapi? Jana ulikuwa na rafiki huyu lakini leo uko na mwingine. Uwezo wa kuwa na mwingine ndio unaoonesha ujasiri wako kwani hukutaka kuvumilia kuwa na mtu ambaye hana nia nzuri na wewe ama faida katika maisha yako.

Binadamu tunatofautiana sana. Haiwezekani ukakutana na mtu ambaye utafanana naye kila kitu lakini unaweza kuwa na mtu au watu ambao mtakuwa na tabia japo chache zinazorandana. Unapokutana na mtu au watu msiowezana hasa kitabia muache mara moja asijekukuumiza kichwa. Jinsi unavyoendelea kubaki naye ndivyo utakavyokwazika ama kuteseka. 

Haijalishi anakupa pesa kiasi gani, mali za thamani, utambulisho kwa watu wazito/vigogo. Kama hakupi furaha, hakuonyeshi upendo, hana muda ma wewe basi fanya hima uachane naye. Tunaishi mara moja, usivumilie ukidhani utabahatika kuwa na "part two" kuishi...mkimbie. Fikiria mara mbili kisha fanya maamuzi sahihi na ya haraka. Unaweza...

Wednesday, June 29, 2016

Usilie sababu kimeisha, tabasamu sababu kilitokea.



Dr Seuss ndiye aliyesema maneno hayo, nami nakazia tu hapo. Tumeumbwa na watu wanaotuzunguka tuishi pamoja tukisaidiana kwa  mambo mbalimbali. Katika kushirikiana katika kazi za kibinaadamu hutokea mengi kama vile kupata wenza na pengine kufika mbali nao kwa kuanzisha familia. 
Maisha ni matamu na yenye furaha tunapozungukwa na watu wenye furaha pia. Wao hutusaidia kujenga amani ndani yetu LAKINI, wanapoondoka sisi huumia sana kwani tunakosa ile furaha tuliyokuwa nayo japo kwa muda tu. 
Tunapofiwa ama kuondokewa na wapendwa wetu kwa sababu za kidunia mfano kusafiri, kuachana, kubadili mitazamo n.k, tunaumia kwani nasi ni binaadamu. Lakini kumbe hatupaswi kulia na kusononeka sababu kila kitu kina sababu. Naye Dr Seuss anatukumbusha hayo kwa kusema tutabasamu kwani walau tulikuwa nao, kutaishi na kufurahi pamoja.

Kuwa na mwanzo mpya. Jipe moyo upate amani kwa afya ya moyo wako. Tabasamu! Tabasamu! Tabasamu!

J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Monday, June 27, 2016

CABBAGE (KABEJI)



Kuna cabbage ya rangi ya kijani na ya damu ya mzee (maroon) ila inaitwa tu nyekundu
Leo tutaangalia faida za cabbage katika miili yetu. Kwanini tuile na inatufaidisha nini?

Mboga hii inatuhusu sana kama wanadamu. Ziangalie faida zifuatazo zitokanazo na ulaji wa kabeji:
  • Ziko za rangi tatu tofauti, kijani, nyeupe na nyekundu. Unanafasi kubwa ya kuchagua ni ya rangi ipi ule. Ya kijani ikikuchosha unakula nyekundu.
  • Haina kiwango kikubwa cha mafuta hivyo hainenepeshi ukiila sana; badala yake inakusaidia kuujenga mwili vizuri sababu ya nyuzi nyuzi zitokanazo na mboga hiyo.
  • Husaidia wajawazito katika kumlinda mtoto awapo tumboni pamoja na kukuza tumbo la mimba bila kuongeza mafuta. Hapo hapo ni chanzo cha folate ambacho ni kipengele kimoja wapo cha DNA (deoxyribonucleic acid-husaidia ugunduzi wa kirithi kwa mwanadamu katika seli (cell) karibuni zote katika mwili); hivyo, huleta uhusiano mzuri wa mama na mtoto.
  • Huipa mifupa na mwili nguvu sababu ya Vitamin C inayoupa mwili nguvu kujiepusha na magonjwa kwa haraka na Vitamin K ambazo husaidia katika kuleta nguvu kwenye mifupa hivyo kusababisha isilegee ama kujikunja. 
  • Inamadini kama Calcium, Potasium, Phosphorus, Manganese, Iron na Magnesium ambayo husaidia kiwango cha moyo na presha ya damu. 
  • Madini ya chuma (Iron) ni muhimu sana sababu huleta chembe chembe nyekundu za damu ambazo husaidia wakina mama wajawazito kutokuwa na upungufu wa damu. 
  • Ni mboga ya msimu. Haivunwi mara kwa mara hivyo inapopatikana ile kwa wingi kabla hujaikosa isipokuwepo.

  • Kabeji nyekundu husaidia kuzuia kansa kwa kuachisha ukuaji/uzalishaji wa seli za cancer.
Kikombe kimoja cha kabeji nyekundu kina 33% ya Vitamin A ambazo tunapaswa kula kila siku.
EMBU ANDAA KABEJI YAKO SASA...

*Waweza iunga kwa kitunguu pekee.
*Waweza ikaanga na chumvi.
*Waweza iunga na kitunguu na nyanya.
*Waweza ipika kwa viungo vyote yaani nyanya, kitunguu, karoti, hoho, pilipili na mazaga mengine unayoyafahamu.
*Waweza ipika kwa karanga au nazi.
*Wengine hupendelea kuiweka kwenye kachumbari. 
*Wale wa diet, inachemswa bila mafuta wala chumvi...kazi kwako!!

J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Friday, June 24, 2016

SHAMBA


Haihitaji kuwa na eneo kubwa ili uanzishe bustani. Bustani ya mboga mboga nyumbani kwako sio tu itakuletea muonekano mzuri wa nyumba yako kwa nje lakini pia, itakusaidia kupata chochote kiendacho kinywani.

Ugumu wa maisha na kupanda na kushuka kwa bei ya vyakula hufanya watu wale mlo mmoja. Lakini unapopata hela ya mboga ukaitunza sababu mboga ziko shambani, basi hiyo akiba unaweza inunulia nyama. Hahah! Hudumia familia yako basi.

Anzisha shamba la matunda na mboga mboga. Anzisha shamba dogo la kile uwezacho. Waweza kuwa na la mchicha au  matembele tu kwa kuanzia. Tunza hela kwa kununua mboga kila siku ambazo unaweza zipata kwako. ZAIDI, utakuwa unapata klilicho salama zaidi


J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Thursday, June 23, 2016

LAKINI SOTE TUNAOGOPA KUSEMA VILIVYO NA THAMANI KUSEMWA...


Hofu ya mwanadamu hutofautiana kwa ukuu. Lakini sote huogopa kwa namna fulani. Hata mwenye nguvu huhofia wenzao wenye.

Tuogope yote lakini tusiogope kusema ukweli inapobidi, na si ukweli tu ila kuzungumza kwa ujumla.

Wapo wenye mawazo mazuri sana ambayo yasipokaliwa kimya yanaweza kuleta athari kubwa tu kwa mtu mmoja au jamii nzima.
Yamkini ukambadilisha mtu / watu, ukaokoa maisha ya mtu / watu, ukapata msaada ulioukusudia au kuutamani kwa muda mrefu, ukatambulika katika familia, ukoo, eneo, nchi, bara au dunia kwa kusema kwako.

Usisite, usikate tamaa, usiogope kusema sababu yule ni mtu mzima, yule ni mkali, yule ni mpole sana, yule haeleweki, yule simuamini. Usihisi labda hivi, labda vile. Sema usikike hata kama utamkwaza, hata kama utamuudhi, hata kama atakujibu vibaya, atakukaripia, atakutukana ama atakukalia kimya. Katika yote, hakika kuna ambalo litamgusa na kumbadilisha japo kidogo.

Kama ni cha thamani kiseme...kitaleta mabadiliko!! Kiseme, moyo wako uridhike pia!!

Katika sehemu ya tatu, kifungu cha 18 cha Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, tunaona kuwa kila mwanadamu anauhuru wa kuongea / kuzungumza. Kumbe basi, ni wajibu wa kila mmoja kuzungumza kile anachoona ni sahihi, ilimradi tu asiseme uongo wala kuzusha jambo.

Usiogope!!

JINSI YA KUPIKA KATLESI


MAHITAJI
  • Viazi ulaya
  • Nyama ya kusagwa
  • Kitunguu swaumu
  • Kitunguu maji
  • Hoho
  • Karoti
  • Mafuta ya kupikia
  • Mayai
  • Pilipili (ukitaka)
MAANDALIZI
  • Menya viazi
  • Vioshe na maji safi
  • Menya na twanga kitunguu swaumu
  • Katakata viungo vipande vidogo vidogo
  • Pasua majai weka kwenye chombo kisafi kisha koroga na chumvi kwa mbali
MAPISHI
  • Chemcha viazi viive
  • Twanga au ponda ponda vilainike
  • Chemsha nyama na chumvi kwa mbali
  • Ikiishaiva weka kitunguu swaumu, kitunguu maji, hoho, karoti na pilipili ukitaka
  • Changanya viungo vyako kwa pamoja vichanganyike vizuri (hakikisha hakuna maji bali mvuke)
  • Weka viazi ulivyoisha viponda
  • Changanya vyote kwa pamoja
  • Chukua kidogo kidogo mkononi
  • Finyanga kwa urefu
zikiwa tayari kwa kukaangwa
  • Tosa kwenye mayai
  • Kaanga kwenye mafuta ya moto
zimeiva, tayari kwa kuliwa
Karibu mezani...




Wednesday, June 22, 2016

JINSI YA KUPIKA TAMBI ZA KUKAANGWA NA MAINI ROSTI



MAHITAJI
  • Maini
  • Tambi
  • Viazi ulaya
  • Nyanya
  • Kitunguu
  • Karoti
  • Hoho
  • Ndimu
  • Kitunguu swaumu
  • Chumvi
  • Mafuta ya kupikia
  • Sukari
  • Iriki
  • Maji safi
MAANDALIZI
  • Kata maini kwa shepu unayotaka
  • Menya viazi kisha kata kata shepu ya maboksi
  • Osha maini na viazi kwa maji safi
  • Katakata viungo vya kupikia (nyanya, kitunguu, hoho na karoti)
  • Menya vitunguu swaumu kisha twangaa vilainike
  • Menya kisha twanga iriki kama punje tano au sita


JINSI YA KUPIKA
*Maini
  • Chemsha maini kidogo kwa maji uliyooshea
  • Weka chumvi na ndimu kidogo kuleta ladha
  • Maji yakiisha kaukia unaweka pembeni kwenye chombo kingine
  • Weka mafuta kiasi ya kupikia
  • Mafuta yakishachemka unaweka kitunguu mpaka kiwe na rangi ya kahawia
  • Weka nyanya
  • Kaanga kaanga nyanya mpaka ziwe rojorojo
  • Weka viazi kisha geuza geuza
  • Weka kitunguu swaumu 
  • Weka maini uliyoyachemsha


  • Koroga koroga mpaka uone maini yanataka kushikana
  • Weka maji kipimo ukitakacho (ila kwa rosti, weka maji kidogo tu kama nusu kikombe cha chai)
  • Vikiishachemka, unaweka karoti na hoho mwishoni
  • Funika vichemke
  • Baada ya muda kidogo unageuza kisha angalia kama chumvi iko sawa (kama bado unaongeza kidogo kabla ya kuipua)
  • Maini yatakuwa tayari kwa kuliwa
*Tambi
  • Chemsha maji yatokote
  • Weka mafuta  kwenye sufuria motoni
  • Yakiishapata moto, vunja vunja tambi kisha ziweke kwenye mafuta
  • Rusha rusha sufuria kuzigeuza mpaka zibadilike rangi kuwa kahawia (brown)
Tambi baada ya kukaangwa (hazijawekwa maji)
  • Weka maji ya moto yafikie juu kidogo ya tambi zinapoishia kwenye sufuria
  • Weka sukari kidogo na iriki uliyoisha itwanga
  • Funika vichemke
  • Angalia angalia kama zimeiva
  • Maji yakikaribia kuisha unatoa sufuria motoni.





Chakula tayari...
Maji mengi huleta mchuzi
Tambi baada ya kuiva



Rosti (haina mchuzi)
Enjoy!!

Monday, June 20, 2016

Courage isn't having the strength to go on, it is going on when you don't have strength...



Napoleon ndiye aliyesema maneno haya " Ujasiri sio kuwa na nguvu za kusonga mbele ila ni kusonga mbele bila ya kuwa na  nguvu".

Binadamu tunakumbwa na changamoto nyingi sana. Wakati mwingine tunapata shida zinazofururiza mpaka tunajiuliza kama Mungu yupo; tukidhani kumetelekezwa njiani. Napoleon anatukumbusha kuwa na nguvu hasa pale tunapokata tamaa kabisa, kwa kufanya hivyo tutakuwa jasiri. Ewe ndugu, usikate tamaa leo. Onyesha ujasiri wako kwa kusonga mbele hata kama unahisi kuelemewa na mizigo ya dunia. Onyesha ujasiri wako hata kama rafiki zako wote wamekukimbia. Onyesha ujasiri kwa kujikongoja bila kuwa na nguvu kwani ni kwa kufanya hivyo, nguvu zitajitengeneza ndani yako na utafanya mambo makubwa mpaka ujishangae. Kuwa jasiri leo...

JINSI YA KUPIKA VIAZI MBATATA, NYAMA YA KUSAGWA NA UJI WA MUHOGO

MAHITAJI
  • Viazi mbatata (viazi ulaya)
  • Nyama ya kusagwa
  • Unga wa muhogo
  • Nyanya
  • Vitunguu
  • Pili pili hoho
  • Karoti
  • Mafuta ya kupikia
  • Maji safi
  • Chumvi
  • Ndimu
  • Pili pili mtama 
  • Ukwaju

MAANDALIZI



  • Menya viazi
  • Kata size unayotaka ama viache vikiwa vizima
  • Vioshe vizuri kwa maji safi
  • Andaa nyanya, vitunguu, hoho na karoti
  • Saga nyama (kama ulinunua ambayo haijasagwa)
  • Kamua ndimu kwenye chombo kidogo
  • Pekecha ukwaju kama unavyotengeneza juisi yake kisha chuja

JINSI YA KUPIKA
*Viazi vya nyama




  • Washa jiko lako
  • Injika sufuria la kupikia jikoni
  • Weka mafuta kwenye sufuria la kupikia
  • Mafuta yakichemka mwaga vitunguu na geuza viive
  • Weka ziazi mbatata kwenye mchanganyiko wako
  • Koroga kwa muda wa dakika kama kumi hivi, mpaka viungulie
  • Tia nyanya na funika ichemke haraka
  • Baada ya dakika moja, funua na geuza
  • Weka nyama ikiwa bado mbichi
  • Nyunyiza mchuzi wa ndimu uliyoisha kamua ili kutoa harufu ya shombo ya ubichi wa nyama
  • Geuza geuza mchanganyiko wako uchanganyike vizuri
  • Acha vichemke kwa dakika kama tano kisha geuza tena
  • Weka hoho na karoti kwa pamoja kisha funika
  • Baada ya dakika tano (kwa moto mdogo usiounguza), funua na koroga vichanganyike vizuri
  • Epua


  • *Uji
    • Bandika maji
    • Acha yachemke yawe vuguvugu
    • Koroga unga kiasi kwenye chombo chenye maji (kama unavyokoroga ugali)
    • Mwaga mchanganyiko ndani ya maji yanayochemka jikoni
    • Acha vichemke kama unavyopika ugali
    • Vikiisha kuchemka, weka ukwaju kidogo kuleta ladha (ikizidi inakuwa chachu)
    • Weka sukari iivie (pima kulingana na uji uliopika
    • Malizia kwa kuweka pilipili mtama kidogo



    Mlo mwema...

    Thursday, June 16, 2016

    Fanya kazi kwa bidii, kuwa na furaha, na tengeneza historia


    Anaitwa Jeff, anasema fanya kazi kwa bidii...lakini si kazi tu, furahi pia na anamalizia kwa kusema tengeneza historia.
    Toka uzaliwe, ni nini umefanya kutengeneza historia? Umefikiria ni nini utaacha kama kumbukumbu ukifa leo?!? Watu wengi wanaaga dunia lakini wachache wanakumbukwa na ulimwengu huku wengine wakikumbukwa na familia zao tu. Kufanya kazi ni wajibu wa kila mtu lakini hakikisha unafurahia kazi uifanyayo ili iwasaidie wengi zaidi ya wewe pekee (oneself). Kwa kufanya hivyo utajenga ukuta imara kati yako na wanaokuzunguka na pengine zaidi za hapo kwa kuujumlisha ulimwengu. TENGENEZA HISTORIA SASA....

    Wednesday, June 15, 2016

    Maisha ya baadaye mali ya yule anayejiandaa leo.

    The Future belongs to those who prepare for it......

    Haya ni maneno ya mwanahistoria mmoja anayefahamika kwa jina la Malcom X.


    Ndugu, ukitaka maisha mazuri ya baadaye sharti ujiandae leo hii. Anza leo, usingoje kesho usiyokuwa na uhakika nayo. Watu wengi hupenda kusubiria kupata mtaji kamili ndipo waanze biashara. wengine husubiri wapate mtoto ndipo wajifunze kulea. wengine wanasubiri mitihani ikaribie ndipo waanze kusoma, wengine wanasubiri shida ndipo wamkumbuke Mungu, wengine hutaka kupunguza miili yao kwa afya njema lakini wanasema "nitaanza kesho au mwezi ujao au tarehe moja (nayo haifiki)". Tusiwe watu wa kusubiri....tuanze sasa. Chochote ulichonacho kiwe kingi au kidogo, anza nacho. UKITAKA MAZURI YA BAADAYE SHARTI UJIANDAE MAPEMA.

    J. A. Y

    Ninajijali, wewe je?

    Tuesday, June 14, 2016

    JINSI YA KUPIKA FUTARI YA MIHOGO NA SAMAKI


    MAHITAJI:
    • Mihogo
    • Nazi
    • Chumvi
    • Samaki
    • Limao/ndimu
    • Mafuta

    *Pilipili manga
    *Kitunguu swaumu
    *Tangawizi

    JINSI YA KUPIKA:
    • Mihogo

    Menya mihogo
    Kata kata vipande vidogo vidogo
    Bandika jikoni
    Acha kwenye moto kwa dakika kumi kama unatumia gesi
    Andaa nazi
    Mimina nazi kwenye mihogo ikiwa bado inachemka
    Tia chumvi kidogo
    Acha vitokote kwa dakika kumi nyingine ili nazi ichemke
    Bonyeza kwa mwiko uone kama imelainika 
    Kama imelainika epua, kama bado ongeza maji kidogo ili iive

    • Samaki

    Andaa samaki wako kwa kuwaparua na kuwaosha vizuri
    Wakate msitari kila upande
    Pakaa chumvi na limao/ndimu
    Pakaa viungo vingine kama pilipili manga, swaumu na tangawizi (ukipenda)
    Weka mafuta kwenye kikaangio
    Injika mafuta kwenye moto yachemke
    Kaanga samaki mpaka wawe na rangi ya kahawia
    Epua

    Waweza kuipamba sahani uliyopakulia chakula chako kwa kachumbari na limao/ndimu kwa ajili ya kuongeza ladha zaidi wakati wa kula.

    Nakutakia mlo mwema....