Monday, July 4, 2016

MAZOEZI SI HAKIKA YA AFYA NJEMA



Mazoezi ni muhimu kwa kukuweka mwenye nguvu muda wote lakini maisha unavyoyaishi pia yanachangia katika kukufanya mwenye furaha, mchangamfu na mwenye afya njema.

Dr. Denis Nturibi anasema kuna vitu vitatu ambavyo binadamu wote tunapaswa kuvifuata ili kuwa na afya njema. Mazoezi ni sahihi kuyafanya lakini muundo wa maisha (lifestyle) yetu unamchango mkubwa pia.

1. Kula sahihi.
Tunapaswa kupata lishe bora kwa maana kwamba tuachane na vyakula ambavyo vinanenepesha hasa vyenye mafuta mengi na sukari nyingi. Tusile sana yaani tule kwa kiwango na kwa muda tu. Kuna watu wanakula kwa siku hata zaidi ya mara nne. Kila unachoona unataka uonje. Basi tujitahidi kujiwekea mipaka yaani nini kiliwe na kwa muda na kiwango gani, Bila kusahau maji ya kunywa (angalau lita moja kwa siku).

2. Pumzika na lala.
Tunafanya kazi kupata hela, sawa kabisa. Hata Mungu anatuambia tufanye kazi na ametuweka duniani hasa kufanya kazi bila hivyo hatupati kula. Lakini kila kitu kiwe kwa kiasi. Pata muda wa kutosha wa kupumzika. Kazi nyingi zinatufanya tutumie akili sana katika kufikiria, kusuluhisha na kudadavua mambo kitu ambacho huchosha sana akili na mwili pia. 
Lala masaa yanayotakiwa (8-10). Usitumie muda mwingi kuangalia luninga ukakesha asubuhi unaelekea darasani au ofisini. Usisome masaa tisa ukalala kwa saa moja au kuvusha kabisa halafu uingie kufanya mtihani. Pumzika  na lala ili akili pia ipumzike na mwili kwa ujumla.

3. Shughuli za kimwili.
Mazoezi ya viungo ni muhimu katika kukufanya mwepesi. Kimbia taratibu (jogging) au tembea kwa mwendo wa haraka kwa umbali kidogo kila siku au walau mara mbili kwa wiki. Hii itakusaidia kukupa pumzi nzuri. Kwa wale waimbaji, sauti yako itapunguza kuhema hema.


Kwahiyo, Dr. Dennis anaeleza vizuri kuwa, mazoezi pekee si afya, lishe na kupumzika pamoja na kulala vinasaidia kwa afya bora.

Unaweza kuwa na mwili mdogo na wenye nguvu sababu ya mazoezi lakini kama unakunywa pombe sana au unavuta sigara utakuwa na nguvu bila afya njema.

Jitengenezee mazingira mzuri ya kuwa na afya muda wote kwani afya njema ndio kila kitu.




No comments:

Post a Comment