Showing posts with label TAMBUA. Show all posts
Showing posts with label TAMBUA. Show all posts

Wednesday, July 20, 2016

Onyesha heshima hata kwa watu wasiostahili; sio kwa muonekano wa tabia zao ila muonekano wa yako.


Maneno ya Dave Willis yanakumbushia utoaji wa heshima. Waswahili wanasema "heshima ni kitu cha bure" yaani huhitaji kulipia wala kugharamia chochote kuheshimu ama kuheshimiwa ila kujiheshimu na kutoa heshima hiyo kwa wengine wote hata kama hawastahili heshima yako.

Inakuwaje mtu hastahili heshima yako? Ni kwa sababu haonyeshi upendo kwako kama binadamu, sababu anakuona uko chini sana, sababu anakudharau, anakuona hufai kwake na katika maisha yake, sababu huna uwezo kifedha ama kifikra, sababu huwezi kufika alipofika, sababu hujampa alichotaka, hauna muonekano mzuri na mengine mengi.

Zipo sababu nyingi lakini pamoja na yote tunapaswa kukumbuka kuwa sote ni binadamu na tunakosea. Inawezekana tukapishana leo  lakini tukumbuke dunia huzunguka, binadamu pia. Tuheshimiane kwani hatujui ya kesho, inawezekana ukamheshimu mtu leo hata kama hastahili na kesho akawa msaada mkubwa tu kwako. Lakini tukijikweza leo, kesho tutaaibika.

Usimuhemu huyu ukamuacha yule ukidhani unakuwa mwema zaidi. Heshimu wote ili uonekane mwenye heshima.

Tuesday, July 12, 2016

AFYA ni nini?


Afya ni hali ya kutokuwa na ugonjwa au kidonda. Afya ni hali ya kuwa na amani ya roho. Afya ni ubora wa akili, mwili na nafsi. Afya hutegemea vitu hivi vitatu kuwa ili kuwa hai na salama:
  • Akili
  • Mwili
  • Nafsi
Akili ni utashi tuliopewa na Mwenyezi Mungu katika kung'amua mambo ulimwenguni. Akili hujumuisha uelewa, ufikiri, uamuzi na utendaji wa mambo. Hakuna awezaye kutafsiri akili yetu ila matendo yetu yanaweza kumfanya mtu aone flani yuko vipi; nayo bado itakuwa mtazamo wake sababu tunatofautiana kufikiri pia. 

Binadamu hutumia akili kila siku na kila wakati ili kuelewa, kufikiri, kuamua na kuhakikisha tunatimiza jambo. Kwa maana hiyo, tunapaswa kuipumzisha "PUMZISHA AKILI". Akili ikichoka mwili nao huchoka na hutafanya chochote sababu haitakuwa na uwezo mzuri kutenda. Lala au oga au ogelea au sikiliza mziki au chochote ukipendacho ambacho hakitakufanya utumie nguvu ya akili.

Mwili ni muundo wote wa binaadam. Ni maumbile ya mtu. Mwili huhusisha yote yaliyotengeneza "mtu" mfano viungo kama miguu, mikono n.k, Maji kama mate, damu n.k, na vingine kama mishipa kucha na nywele.

Tunapaswa kujipenda kwa kula vizuri, kulala vizuri na pazuri, kuvaa vizuri na kujijali muda wote kwa kuuweka mwili salama mfano kwa kupiga mswaki baada ya kula, kuosha nywele mara kwa mara, kukata na kusafisha kucha, kuoga, na kuvaa nguo safi. Pia tujiepushe na hatari, ugomvi na makwazo kwa faida ya mioyo yetu. 

Ukitembea sana juani pata kivuli unywe na maji. Penye baridi uvike mwili wako kwa sweta ama nguo nzito. Ukiumia au kuumwa pata matibabu sahihi kwa kwenda hospitalini. Jipende, Ujali mwili wako. Tukifanya hivyo miili yetu itakuwa salama. 

Nafsi ni roho yenye kuleta imani ndani yetu. Sisi huamini vitu mbali mbali kwa msaada wa nafsi. Lakini yote heri kama tutaamini vitu vyenye kujenga na sio kubomoa. Nafsi pia hutofautiana ya mtu na mwingine ndio maana tukawa tofauti japo chimbuko letu kiuumbaji ni moja. 

Nafsi nayo huhitaji utulivu ili kuupa mwili na akili nguvu za kuishi kwa afya. Pata muda wa kutulia ukiongea na WEWE kujua nini waweza fanya LAKINI, mshirikishe MUUMBA wako kwa yote kupata amani uitakayo moyoni na kwa wakuzungukao.

Hivyo basi, jipe likizo au omba likizo. Tembelea sehemu mbali mbali za starehe au vivutio kutuliza mwili, akili na roho pia. Ongea vizuri na watu, cheka, tabasamu hata kama umeumizwa. Inasaidia sana. 

Afya ya vitu vyote vitatu ni muhimu katika kukuweka mwenye nguvu na furaha.
 Jali afya yako!



Monday, July 4, 2016

MAZOEZI SI HAKIKA YA AFYA NJEMA



Mazoezi ni muhimu kwa kukuweka mwenye nguvu muda wote lakini maisha unavyoyaishi pia yanachangia katika kukufanya mwenye furaha, mchangamfu na mwenye afya njema.

Dr. Denis Nturibi anasema kuna vitu vitatu ambavyo binadamu wote tunapaswa kuvifuata ili kuwa na afya njema. Mazoezi ni sahihi kuyafanya lakini muundo wa maisha (lifestyle) yetu unamchango mkubwa pia.

1. Kula sahihi.
Tunapaswa kupata lishe bora kwa maana kwamba tuachane na vyakula ambavyo vinanenepesha hasa vyenye mafuta mengi na sukari nyingi. Tusile sana yaani tule kwa kiwango na kwa muda tu. Kuna watu wanakula kwa siku hata zaidi ya mara nne. Kila unachoona unataka uonje. Basi tujitahidi kujiwekea mipaka yaani nini kiliwe na kwa muda na kiwango gani, Bila kusahau maji ya kunywa (angalau lita moja kwa siku).

2. Pumzika na lala.
Tunafanya kazi kupata hela, sawa kabisa. Hata Mungu anatuambia tufanye kazi na ametuweka duniani hasa kufanya kazi bila hivyo hatupati kula. Lakini kila kitu kiwe kwa kiasi. Pata muda wa kutosha wa kupumzika. Kazi nyingi zinatufanya tutumie akili sana katika kufikiria, kusuluhisha na kudadavua mambo kitu ambacho huchosha sana akili na mwili pia. 
Lala masaa yanayotakiwa (8-10). Usitumie muda mwingi kuangalia luninga ukakesha asubuhi unaelekea darasani au ofisini. Usisome masaa tisa ukalala kwa saa moja au kuvusha kabisa halafu uingie kufanya mtihani. Pumzika  na lala ili akili pia ipumzike na mwili kwa ujumla.

3. Shughuli za kimwili.
Mazoezi ya viungo ni muhimu katika kukufanya mwepesi. Kimbia taratibu (jogging) au tembea kwa mwendo wa haraka kwa umbali kidogo kila siku au walau mara mbili kwa wiki. Hii itakusaidia kukupa pumzi nzuri. Kwa wale waimbaji, sauti yako itapunguza kuhema hema.


Kwahiyo, Dr. Dennis anaeleza vizuri kuwa, mazoezi pekee si afya, lishe na kupumzika pamoja na kulala vinasaidia kwa afya bora.

Unaweza kuwa na mwili mdogo na wenye nguvu sababu ya mazoezi lakini kama unakunywa pombe sana au unavuta sigara utakuwa na nguvu bila afya njema.

Jitengenezee mazingira mzuri ya kuwa na afya muda wote kwani afya njema ndio kila kitu.




Monday, June 27, 2016

CABBAGE (KABEJI)



Kuna cabbage ya rangi ya kijani na ya damu ya mzee (maroon) ila inaitwa tu nyekundu
Leo tutaangalia faida za cabbage katika miili yetu. Kwanini tuile na inatufaidisha nini?

Mboga hii inatuhusu sana kama wanadamu. Ziangalie faida zifuatazo zitokanazo na ulaji wa kabeji:
  • Ziko za rangi tatu tofauti, kijani, nyeupe na nyekundu. Unanafasi kubwa ya kuchagua ni ya rangi ipi ule. Ya kijani ikikuchosha unakula nyekundu.
  • Haina kiwango kikubwa cha mafuta hivyo hainenepeshi ukiila sana; badala yake inakusaidia kuujenga mwili vizuri sababu ya nyuzi nyuzi zitokanazo na mboga hiyo.
  • Husaidia wajawazito katika kumlinda mtoto awapo tumboni pamoja na kukuza tumbo la mimba bila kuongeza mafuta. Hapo hapo ni chanzo cha folate ambacho ni kipengele kimoja wapo cha DNA (deoxyribonucleic acid-husaidia ugunduzi wa kirithi kwa mwanadamu katika seli (cell) karibuni zote katika mwili); hivyo, huleta uhusiano mzuri wa mama na mtoto.
  • Huipa mifupa na mwili nguvu sababu ya Vitamin C inayoupa mwili nguvu kujiepusha na magonjwa kwa haraka na Vitamin K ambazo husaidia katika kuleta nguvu kwenye mifupa hivyo kusababisha isilegee ama kujikunja. 
  • Inamadini kama Calcium, Potasium, Phosphorus, Manganese, Iron na Magnesium ambayo husaidia kiwango cha moyo na presha ya damu. 
  • Madini ya chuma (Iron) ni muhimu sana sababu huleta chembe chembe nyekundu za damu ambazo husaidia wakina mama wajawazito kutokuwa na upungufu wa damu. 
  • Ni mboga ya msimu. Haivunwi mara kwa mara hivyo inapopatikana ile kwa wingi kabla hujaikosa isipokuwepo.

  • Kabeji nyekundu husaidia kuzuia kansa kwa kuachisha ukuaji/uzalishaji wa seli za cancer.
Kikombe kimoja cha kabeji nyekundu kina 33% ya Vitamin A ambazo tunapaswa kula kila siku.
EMBU ANDAA KABEJI YAKO SASA...

*Waweza iunga kwa kitunguu pekee.
*Waweza ikaanga na chumvi.
*Waweza iunga na kitunguu na nyanya.
*Waweza ipika kwa viungo vyote yaani nyanya, kitunguu, karoti, hoho, pilipili na mazaga mengine unayoyafahamu.
*Waweza ipika kwa karanga au nazi.
*Wengine hupendelea kuiweka kwenye kachumbari. 
*Wale wa diet, inachemswa bila mafuta wala chumvi...kazi kwako!!

Friday, June 24, 2016

SHAMBA


Haihitaji kuwa na eneo kubwa ili uanzishe bustani. Bustani ya mboga mboga nyumbani kwako sio tu itakuletea muonekano mzuri wa nyumba yako kwa nje lakini pia, itakusaidia kupata chochote kiendacho kinywani.

Ugumu wa maisha na kupanda na kushuka kwa bei ya vyakula hufanya watu wale mlo mmoja. Lakini unapopata hela ya mboga ukaitunza sababu mboga ziko shambani, basi hiyo akiba unaweza inunulia nyama. Hahah! Hudumia familia yako basi.

Anzisha shamba la matunda na mboga mboga. Anzisha shamba dogo la kile uwezacho. Waweza kuwa na la mchicha au  matembele tu kwa kuanzia. Tunza hela kwa kununua mboga kila siku ambazo unaweza zipata kwako. ZAIDI, utakuwa unapata klilicho salama zaidi


Thursday, June 23, 2016

JINSI YA KUPIKA KATLESI


MAHITAJI
  • Viazi ulaya
  • Nyama ya kusagwa
  • Kitunguu swaumu
  • Kitunguu maji
  • Hoho
  • Karoti
  • Mafuta ya kupikia
  • Mayai
  • Pilipili (ukitaka)
MAANDALIZI
  • Menya viazi
  • Vioshe na maji safi
  • Menya na twanga kitunguu swaumu
  • Katakata viungo vipande vidogo vidogo
  • Pasua majai weka kwenye chombo kisafi kisha koroga na chumvi kwa mbali
MAPISHI
  • Chemcha viazi viive
  • Twanga au ponda ponda vilainike
  • Chemsha nyama na chumvi kwa mbali
  • Ikiishaiva weka kitunguu swaumu, kitunguu maji, hoho, karoti na pilipili ukitaka
  • Changanya viungo vyako kwa pamoja vichanganyike vizuri (hakikisha hakuna maji bali mvuke)
  • Weka viazi ulivyoisha viponda
  • Changanya vyote kwa pamoja
  • Chukua kidogo kidogo mkononi
  • Finyanga kwa urefu
zikiwa tayari kwa kukaangwa
  • Tosa kwenye mayai
  • Kaanga kwenye mafuta ya moto
zimeiva, tayari kwa kuliwa
Karibu mezani...




Wednesday, June 22, 2016

JINSI YA KUPIKA TAMBI ZA KUKAANGWA NA MAINI ROSTI



MAHITAJI
  • Maini
  • Tambi
  • Viazi ulaya
  • Nyanya
  • Kitunguu
  • Karoti
  • Hoho
  • Ndimu
  • Kitunguu swaumu
  • Chumvi
  • Mafuta ya kupikia
  • Sukari
  • Iriki
  • Maji safi
MAANDALIZI
  • Kata maini kwa shepu unayotaka
  • Menya viazi kisha kata kata shepu ya maboksi
  • Osha maini na viazi kwa maji safi
  • Katakata viungo vya kupikia (nyanya, kitunguu, hoho na karoti)
  • Menya vitunguu swaumu kisha twangaa vilainike
  • Menya kisha twanga iriki kama punje tano au sita


JINSI YA KUPIKA
*Maini
  • Chemsha maini kidogo kwa maji uliyooshea
  • Weka chumvi na ndimu kidogo kuleta ladha
  • Maji yakiisha kaukia unaweka pembeni kwenye chombo kingine
  • Weka mafuta kiasi ya kupikia
  • Mafuta yakishachemka unaweka kitunguu mpaka kiwe na rangi ya kahawia
  • Weka nyanya
  • Kaanga kaanga nyanya mpaka ziwe rojorojo
  • Weka viazi kisha geuza geuza
  • Weka kitunguu swaumu 
  • Weka maini uliyoyachemsha


  • Koroga koroga mpaka uone maini yanataka kushikana
  • Weka maji kipimo ukitakacho (ila kwa rosti, weka maji kidogo tu kama nusu kikombe cha chai)
  • Vikiishachemka, unaweka karoti na hoho mwishoni
  • Funika vichemke
  • Baada ya muda kidogo unageuza kisha angalia kama chumvi iko sawa (kama bado unaongeza kidogo kabla ya kuipua)
  • Maini yatakuwa tayari kwa kuliwa
*Tambi
  • Chemsha maji yatokote
  • Weka mafuta  kwenye sufuria motoni
  • Yakiishapata moto, vunja vunja tambi kisha ziweke kwenye mafuta
  • Rusha rusha sufuria kuzigeuza mpaka zibadilike rangi kuwa kahawia (brown)
Tambi baada ya kukaangwa (hazijawekwa maji)
  • Weka maji ya moto yafikie juu kidogo ya tambi zinapoishia kwenye sufuria
  • Weka sukari kidogo na iriki uliyoisha itwanga
  • Funika vichemke
  • Angalia angalia kama zimeiva
  • Maji yakikaribia kuisha unatoa sufuria motoni.





Chakula tayari...
Maji mengi huleta mchuzi
Tambi baada ya kuiva



Rosti (haina mchuzi)
Enjoy!!

Monday, June 20, 2016

JINSI YA KUPIKA VIAZI MBATATA, NYAMA YA KUSAGWA NA UJI WA MUHOGO

MAHITAJI
  • Viazi mbatata (viazi ulaya)
  • Nyama ya kusagwa
  • Unga wa muhogo
  • Nyanya
  • Vitunguu
  • Pili pili hoho
  • Karoti
  • Mafuta ya kupikia
  • Maji safi
  • Chumvi
  • Ndimu
  • Pili pili mtama 
  • Ukwaju

MAANDALIZI



  • Menya viazi
  • Kata size unayotaka ama viache vikiwa vizima
  • Vioshe vizuri kwa maji safi
  • Andaa nyanya, vitunguu, hoho na karoti
  • Saga nyama (kama ulinunua ambayo haijasagwa)
  • Kamua ndimu kwenye chombo kidogo
  • Pekecha ukwaju kama unavyotengeneza juisi yake kisha chuja

JINSI YA KUPIKA
*Viazi vya nyama




  • Washa jiko lako
  • Injika sufuria la kupikia jikoni
  • Weka mafuta kwenye sufuria la kupikia
  • Mafuta yakichemka mwaga vitunguu na geuza viive
  • Weka ziazi mbatata kwenye mchanganyiko wako
  • Koroga kwa muda wa dakika kama kumi hivi, mpaka viungulie
  • Tia nyanya na funika ichemke haraka
  • Baada ya dakika moja, funua na geuza
  • Weka nyama ikiwa bado mbichi
  • Nyunyiza mchuzi wa ndimu uliyoisha kamua ili kutoa harufu ya shombo ya ubichi wa nyama
  • Geuza geuza mchanganyiko wako uchanganyike vizuri
  • Acha vichemke kwa dakika kama tano kisha geuza tena
  • Weka hoho na karoti kwa pamoja kisha funika
  • Baada ya dakika tano (kwa moto mdogo usiounguza), funua na koroga vichanganyike vizuri
  • Epua


  • *Uji
    • Bandika maji
    • Acha yachemke yawe vuguvugu
    • Koroga unga kiasi kwenye chombo chenye maji (kama unavyokoroga ugali)
    • Mwaga mchanganyiko ndani ya maji yanayochemka jikoni
    • Acha vichemke kama unavyopika ugali
    • Vikiisha kuchemka, weka ukwaju kidogo kuleta ladha (ikizidi inakuwa chachu)
    • Weka sukari iivie (pima kulingana na uji uliopika
    • Malizia kwa kuweka pilipili mtama kidogo



    Mlo mwema...

    Tuesday, June 14, 2016

    JINSI YA KUPIKA FUTARI YA MIHOGO NA SAMAKI


    MAHITAJI:
    • Mihogo
    • Nazi
    • Chumvi
    • Samaki
    • Limao/ndimu
    • Mafuta

    *Pilipili manga
    *Kitunguu swaumu
    *Tangawizi

    JINSI YA KUPIKA:
    • Mihogo

    Menya mihogo
    Kata kata vipande vidogo vidogo
    Bandika jikoni
    Acha kwenye moto kwa dakika kumi kama unatumia gesi
    Andaa nazi
    Mimina nazi kwenye mihogo ikiwa bado inachemka
    Tia chumvi kidogo
    Acha vitokote kwa dakika kumi nyingine ili nazi ichemke
    Bonyeza kwa mwiko uone kama imelainika 
    Kama imelainika epua, kama bado ongeza maji kidogo ili iive

    • Samaki

    Andaa samaki wako kwa kuwaparua na kuwaosha vizuri
    Wakate msitari kila upande
    Pakaa chumvi na limao/ndimu
    Pakaa viungo vingine kama pilipili manga, swaumu na tangawizi (ukipenda)
    Weka mafuta kwenye kikaangio
    Injika mafuta kwenye moto yachemke
    Kaanga samaki mpaka wawe na rangi ya kahawia
    Epua

    Waweza kuipamba sahani uliyopakulia chakula chako kwa kachumbari na limao/ndimu kwa ajili ya kuongeza ladha zaidi wakati wa kula.

    Nakutakia mlo mwema....

    Friday, May 27, 2016

    HUDUMA YA KWANZA

    Tumbo la kuhara

    Ni matumaini yangu hakuna mtu ambaye hajawahi kuumwa tumbo hata siku moja toka azaliwe. Lakini leo naongelea kuvurugwa kwa tumbo. Yawezekana ukawa umepata chakula mchnaganyiko ama vinywaji tofauti ambavyo vikasababisha kuvurugika kwa tumbo. Inawezekana ukawa umetoka sehemu moja kwenda nyingine yaani kubadilika kwa mazingira, hivyo kuhisi umevurugika tumbo. Lakini pia yawezekana ukawa unahofu sana kutokana na kusubiri matokeo fulani kama ya mtihani kimasomo ama majibu ya daktari ama ya usaili wa kazi. Yote haya na mengine mengi husababisha kuvurugika kwa tumbo na mara nyingi kupelekea kutaka kuhara (kuharisha).

    Mvurugiko huu wa tumbo humfanya mtu kukosa raha na hasa pale anapokuwa nje ya mazingira ya nyumbani ama sehemu iliyo karibu na huduma ya choo. Unachoweza kufanya ni kutafuta dawa ya kuzuia kuharisha kwenye maduka ya dawa yaliyoko karibu na wewe. LAKINI, si mara zote itawezekana kuwa hivyo, basi nini kifanyike unapokosa dawa hizo?

    Ukiwa nyumbani, chukua sukari na chumvi kisha chota chumvi kijiko kidogo cha chai nusu uweke kwenye kikombe na kiasi hicho hicho chota sukari uweke. Baada ya hapo changanya na maji kidogo sana ili kuepuka kupoteza ladha ya ukali dawa hiyo. Kwa kuwa uliweka kijiko kidogo nusu basi maji yaweke kiwango cha vijiko vikubwa vya kulia chakula vitano au sita. Koroga mchanganyiko wa chumvi na sukari kisha kunywa yote bila kuisikilizia. Tumbo litakata maumivu na dalili za kuhara mara moja. Na kama uliishaanza kuhara basi hali hiyo itaisha.

    Ukiwa nje ya mazingira ya nyumbani na hujapata msaada wowote wa chumvi na sukari ama dawa basi tafuta maji safi ya kunywa walau lita moja kisha vuta pumzi ndani na nje kwa nguvu kwa muda wa dakika tatu mpaka tano. 

    Friday, April 22, 2016

    MoYo


    Je, unaufahamu kuwa kila mwanadamu anapumua kwa msaada wa moyo? Na je, unafahamu kuwa moyo huo huo unaweza kumfanya mtu kuwa na furaha ama huzuni? 

    Hii ni alama ambayo wengi huitumia kuashiria moyo na moyo huo basi unatumika kama ishara ya upendo. 
    Moyo ni pampu inayosukuma damu kupitia mishipa ya damu. Kupitia mishipa hiyo damu husambazwa mwili mzima ili kukupatia hewa safi (oxygen). Tukiachana na maswala ya kibaiolojia, moyo unakazi ya kupenda.

    Basi tuone upendo huo unaathiri vipi moyo na wewe kama binadamu unaukosea vipi moyo wako ama moyo wa mwingine. Jijali, mjali na mwenzio ili kuufurahisha moyo kwa afya zaidi. 



    Huu ni moyo wa binadamu. 
    Unapokuwa umezungukwa na watu wakupendao haijalishi ni upendo wa aina gani, moyo huwa na nguvu na hufanya kazi yake vizuri. Kila mmoja anapenda kupendwa, hata wababe huwa na wafuasi wao hata kama hawana upendo wa dhati.
    Moyo wenye furaha. 
    Moyo wenye nguvu

    Moyo wenye furaha huimba ndani yetu pale tunapoongeza marafiki wapya. Moyo wenye furaha huupoza mwili tusikiapo baridi yaani tuwapo wapweke, kwa kukumbuka mema mengi yaliyopita. Inawezekana kabisa kwa wewe kujichangamsha bila kusubiri kuchangamshwa.

    Moyo imara ni moyo wenye nguvu kwani unaweza kupigana na majaribu yote yanayotukumba katika maisha. Sisi sote tunapaswa kuwa na moyo wenye nguvu kwani pia ni rahisi kupingana na magonjwa tukianza na ugonjwa wa 'moyo' wenyewe.

    Upendo wa nguvu
    Upendo wa mahusiano ya kimapenzi ni upendo unaoleta hisia za kipekee. Kila mmoja anaweza kuuelezea ajuavyo yeye. LAKINI, maumivu ya kuachana kwa wapenzi hao yanaweza kuwa yanafanana kwani yote huumiza moyo.

    Upendo unaolega lega
    Afya ya mtu ni ya thamani, ni vema kutumia nafasi unayopata kwa mpenzi wako kumuonesha upendo na kupata upendo kutoka kwake. Kama unadhani hujaamua bado kujiingiza kwenye mahusiano, basi tafakari kabla ya kuchukua hatua. Ni vema kujiamini kwa ulifanyalo kuepukana na maumivu ya moyo. Kipindi tu unapojihusisha na mahusiano ya kimapenzi, fahamu kuwa unajifunga. 

    Moyo uliofungwa kwa upendaye,
    usiufungulie kwa wengine. 
    Angalizo: Ili kuulinda moyo (wako/mwemzako) na maumivu zingatia haya:-
    • usiruhusu mtu kukuzoea haraka
    • usitoe siri zako 
    • usiseme udhaifu wako 
    • usijihakikishie mahusiano marefu (ingawa inapaswa kuwa hivyo)
    • usimchagulie mtu mpenzi
    • usimlazimishe mtu kukupenda
    • usijilazimishe kumpenda mtu
    • usimtumie mtu kama njia ya kumsahau aliyekuumiza
    • usiogope kumuambia unampenda (kama ndio mmeonana) bila kujali wewe ni ME au KE.
    • usipoteze muda mwingi kujifikiria juu ya jibu la kutoa 
    • usianzishe mahisiano mengine wakati uliyonayo sasa hayajaisha
    • usiwe mkimya sana wala mchangamfu kupita kiasi (utaboa)
    • usisubiri kutafutwa, anza pia (usitegee)
    • usingoje kusaidiwa, saidia pia (ushirikiano)
    • usiwe mkali sana ama mbabe kwa mwenzio
    • mkumbatie kwa muda mrefu kila upatapo nafasi (kumbato husaidia kuondoa huzuni kwa kiasi fulani lakini pia huzidisha ukaribu)
    • mpatie zawadi ndogo ndogo (mfanye atabasamu)
    • mchekeshe kwa vistori na michejo
    • muombe msamaha hata kama amekosa yeye
    • mwambie unampenda mara kwa mara
    • usijaribu mahusiano na mtu mwenye mahusiano
    Ukipata mwenzako mshikilie sawa sawa
    Ni bora kuumia kidole kitapona au kuvunjika kidole vingine vitafanya kazi lakini sio kuumia moyo sababu maumivu yake yaweza kuchukua miaka kuisha na kuvunjika kwa moyo ni ngumu kuutengeneza ukafanya kazi sawia.
    Moyo usioweza
    kufanya maamuzi
    sahihi
    Moyo ulionyong'onyea
    na kudhoofika
    Moyo
    uliochanganyikiwa.
    Hapa ndipo tunaposhauriwa kuwa na imani kwa kumuomba Mungu kwani yeye ndiye aliyekupa maisha. Jijali kwa kuepukana na athari hizo lakini pia, kama ikitokea ushaumizwa basi jitahidi kujishughulisha sana ili kupunguza mawazo. Kaa na watu watakupa mawazo tofauti usikae mwenyewe ukiwa mpweke kuepukana na mawazo potofu. Kemea roho ndani yako inayokusukuma kukata tamaa, kuchukia ama kujiua. Sali sana ukisikia hivyo kwa afya ya Roho na moyo pia.

    Maumivu makali ya moyo 
    Usiuzeeshe moyo wako kwa mambo usiyoyaweza. Usiukondeshe kwa kuupa mambo mengi usiyoweza kuyafuatilia na kuyafanya kwa ufanisi, usiufanye ukaelemewa. Ujali moyo wako kwa kujipenda na kuwa makini. Lakini kikubwa, usiutegemee moyo pekee katika mapenzi, shirikisha akili yako. Ni kwa kufanya hivyo, moyo utabaki kupenda tu huku mengine yakifanywa kwa utashi uliobarikiwa nao.

    Thursday, April 21, 2016

    Urefu wa kupindukia

    Wewe ni mrefu? Ni mara ngapi umekutana na watu warefu? Ni nini kinafanya mtu awe mrefu? Fuatilia.....

    Wanabiolojia wa molekuli (molecular biologists) wanaeleza kuwa tofauti ya urefu wa mtu na mtu kwa asilimia 60 mpaka 80 unatokana na maumbile huku asilimia 20 mpaka 40 unatokana na sababu za mazingira hasa lishe.  Urefu wa maumbile sana sana ni ule unaorithiwa hasa kutoka kwa mwanafamilia ama ndugu wa karibu.

    Kila mmoja anahomoni za ukuaji (somatotropin) ambazo zinamsababisha kurefuka haraka ama taratibu. Utofauti huu ndio unaoleta utofauti katika urefu wa mtu na mtu.
    Hizi homoni zina protini 191 zenye amino acid na uzito wa daltoni 22,124; na huzalishwa kwenye glandi iitwayo pituitary ambayo husambaza homini hizo mwilini kwa ajili ya ukuaji mara baada ya uzalishaji wake.

    Wengi wetu tutakumbuka msemo wa wazazi kwa watoto wao wa "lala ukue" kama kumuhamasisha aende kulala hasa wakati wa mchana ambapo watoto wengi hupenda kuutumia kucheza. Inawezekana baadhi wa wazazi wanautumia kama mazoea lakini msemo huo unaukweli ndani yake.

    Usambazaji wa homoni huchukua muda wa masaa matatu hadi matano lakini mtu hurefuka haraka ndani ya lisaa limoja tu akiwa amelala usingizi mzito. Hivyo ukuaji kutokea mara baada ya usambazaji wa homoni zinazohusika na ukuaji. Zikisambaa haraka na kwa wingi ndivyo mtu akuavyo mrefu zaidi kwa kipindi kifupi tu.

    Homoni hizi hufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa watoto na vijana ambao wako katika kipindi cha ukuaji, na si kwa mtu mzima. Wazazi tuwashauri watoto wetu kupata usingizi wa kutosha ili kumsaidia kukua haraka.

    Yamkini hawa ni wapenzi, pamoja na kuwepo kwa tofauti zao kiurefu bado wanaonekana kupendana. (picha kushoto)

    Hawa nao ni marafiki, wao huchweza pamoja mpira wa kikapu. Wanaonekana kuwa wenye furaha sana ukiweka kando ukweli kuwa wamepishana sana urefu. (picha chini kulia)


    Hivyo, kama wewe ni mrefu kuzidi wenzako usijione wa tofauti sana, kaa nao, cheza nao, furahi pamoja nao na wala usijitenge kwani furaha yako ni furaha ya jamii nzima.
    Na kama wewe si mrefu usijishangae pia na wala usimtenge aliye mrefu zaidi yako.

    Kinachofanya mtu awe mkubwa zaidi au mdogo zaidi ni sehemu ya mbele ya glandi ya pituitary iitwayo 'anterior pituitary'. Ikifanya kazi kupita kiwango humfanya mtu kuwa mrefu mno yaani 'giant' na vile vile inapofanya kazi chini ya kiwango basi mtu huwa mfupi zaidi yaani 'dwarf'.

    Ewe kijana, unataka kuwa mrefu? Nawe mzazi, unataka mwanao arefuke vizuri? basi kama uko kwenye umri wa ukuaji bado unayo nafasi. Epukana na vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi (junk food). Pata lishe iliyobora kuisaidia glandi inayohusika na homoni za ukuaji kufanya kazi sahihi katika mwili wako. Hakikisha unapata usingizi wa kutosha ili kurahishisha somatotropin (homoni za ukuaji) kufanya mzunguko vizuri katika mfumo wake.


    Kunywa maziwa ili upate calcium itakayokuimarishia mifupa yako. Urefu ukiambatana na mifupa legevu unaweza kupata matege lakini ukipata calcium basi unakuwa imara muda wote. Kula vyakula vyenye amino acid mfano samaki, mayai, mboga mboga kama mabilinganya na matunda kama karoti matikiti na maepo.