Wednesday, June 29, 2016

Usilie sababu kimeisha, tabasamu sababu kilitokea.



Dr Seuss ndiye aliyesema maneno hayo, nami nakazia tu hapo. Tumeumbwa na watu wanaotuzunguka tuishi pamoja tukisaidiana kwa  mambo mbalimbali. Katika kushirikiana katika kazi za kibinaadamu hutokea mengi kama vile kupata wenza na pengine kufika mbali nao kwa kuanzisha familia. 
Maisha ni matamu na yenye furaha tunapozungukwa na watu wenye furaha pia. Wao hutusaidia kujenga amani ndani yetu LAKINI, wanapoondoka sisi huumia sana kwani tunakosa ile furaha tuliyokuwa nayo japo kwa muda tu. 
Tunapofiwa ama kuondokewa na wapendwa wetu kwa sababu za kidunia mfano kusafiri, kuachana, kubadili mitazamo n.k, tunaumia kwani nasi ni binaadamu. Lakini kumbe hatupaswi kulia na kusononeka sababu kila kitu kina sababu. Naye Dr Seuss anatukumbusha hayo kwa kusema tutabasamu kwani walau tulikuwa nao, kutaishi na kufurahi pamoja.

Kuwa na mwanzo mpya. Jipe moyo upate amani kwa afya ya moyo wako. Tabasamu! Tabasamu! Tabasamu!

J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Monday, June 27, 2016

CABBAGE (KABEJI)



Kuna cabbage ya rangi ya kijani na ya damu ya mzee (maroon) ila inaitwa tu nyekundu
Leo tutaangalia faida za cabbage katika miili yetu. Kwanini tuile na inatufaidisha nini?

Mboga hii inatuhusu sana kama wanadamu. Ziangalie faida zifuatazo zitokanazo na ulaji wa kabeji:
  • Ziko za rangi tatu tofauti, kijani, nyeupe na nyekundu. Unanafasi kubwa ya kuchagua ni ya rangi ipi ule. Ya kijani ikikuchosha unakula nyekundu.
  • Haina kiwango kikubwa cha mafuta hivyo hainenepeshi ukiila sana; badala yake inakusaidia kuujenga mwili vizuri sababu ya nyuzi nyuzi zitokanazo na mboga hiyo.
  • Husaidia wajawazito katika kumlinda mtoto awapo tumboni pamoja na kukuza tumbo la mimba bila kuongeza mafuta. Hapo hapo ni chanzo cha folate ambacho ni kipengele kimoja wapo cha DNA (deoxyribonucleic acid-husaidia ugunduzi wa kirithi kwa mwanadamu katika seli (cell) karibuni zote katika mwili); hivyo, huleta uhusiano mzuri wa mama na mtoto.
  • Huipa mifupa na mwili nguvu sababu ya Vitamin C inayoupa mwili nguvu kujiepusha na magonjwa kwa haraka na Vitamin K ambazo husaidia katika kuleta nguvu kwenye mifupa hivyo kusababisha isilegee ama kujikunja. 
  • Inamadini kama Calcium, Potasium, Phosphorus, Manganese, Iron na Magnesium ambayo husaidia kiwango cha moyo na presha ya damu. 
  • Madini ya chuma (Iron) ni muhimu sana sababu huleta chembe chembe nyekundu za damu ambazo husaidia wakina mama wajawazito kutokuwa na upungufu wa damu. 
  • Ni mboga ya msimu. Haivunwi mara kwa mara hivyo inapopatikana ile kwa wingi kabla hujaikosa isipokuwepo.

  • Kabeji nyekundu husaidia kuzuia kansa kwa kuachisha ukuaji/uzalishaji wa seli za cancer.
Kikombe kimoja cha kabeji nyekundu kina 33% ya Vitamin A ambazo tunapaswa kula kila siku.
EMBU ANDAA KABEJI YAKO SASA...

*Waweza iunga kwa kitunguu pekee.
*Waweza ikaanga na chumvi.
*Waweza iunga na kitunguu na nyanya.
*Waweza ipika kwa viungo vyote yaani nyanya, kitunguu, karoti, hoho, pilipili na mazaga mengine unayoyafahamu.
*Waweza ipika kwa karanga au nazi.
*Wengine hupendelea kuiweka kwenye kachumbari. 
*Wale wa diet, inachemswa bila mafuta wala chumvi...kazi kwako!!

J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Friday, June 24, 2016

SHAMBA


Haihitaji kuwa na eneo kubwa ili uanzishe bustani. Bustani ya mboga mboga nyumbani kwako sio tu itakuletea muonekano mzuri wa nyumba yako kwa nje lakini pia, itakusaidia kupata chochote kiendacho kinywani.

Ugumu wa maisha na kupanda na kushuka kwa bei ya vyakula hufanya watu wale mlo mmoja. Lakini unapopata hela ya mboga ukaitunza sababu mboga ziko shambani, basi hiyo akiba unaweza inunulia nyama. Hahah! Hudumia familia yako basi.

Anzisha shamba la matunda na mboga mboga. Anzisha shamba dogo la kile uwezacho. Waweza kuwa na la mchicha au  matembele tu kwa kuanzia. Tunza hela kwa kununua mboga kila siku ambazo unaweza zipata kwako. ZAIDI, utakuwa unapata klilicho salama zaidi


J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Thursday, June 23, 2016

LAKINI SOTE TUNAOGOPA KUSEMA VILIVYO NA THAMANI KUSEMWA...


Hofu ya mwanadamu hutofautiana kwa ukuu. Lakini sote huogopa kwa namna fulani. Hata mwenye nguvu huhofia wenzao wenye.

Tuogope yote lakini tusiogope kusema ukweli inapobidi, na si ukweli tu ila kuzungumza kwa ujumla.

Wapo wenye mawazo mazuri sana ambayo yasipokaliwa kimya yanaweza kuleta athari kubwa tu kwa mtu mmoja au jamii nzima.
Yamkini ukambadilisha mtu / watu, ukaokoa maisha ya mtu / watu, ukapata msaada ulioukusudia au kuutamani kwa muda mrefu, ukatambulika katika familia, ukoo, eneo, nchi, bara au dunia kwa kusema kwako.

Usisite, usikate tamaa, usiogope kusema sababu yule ni mtu mzima, yule ni mkali, yule ni mpole sana, yule haeleweki, yule simuamini. Usihisi labda hivi, labda vile. Sema usikike hata kama utamkwaza, hata kama utamuudhi, hata kama atakujibu vibaya, atakukaripia, atakutukana ama atakukalia kimya. Katika yote, hakika kuna ambalo litamgusa na kumbadilisha japo kidogo.

Kama ni cha thamani kiseme...kitaleta mabadiliko!! Kiseme, moyo wako uridhike pia!!

Katika sehemu ya tatu, kifungu cha 18 cha Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, tunaona kuwa kila mwanadamu anauhuru wa kuongea / kuzungumza. Kumbe basi, ni wajibu wa kila mmoja kuzungumza kile anachoona ni sahihi, ilimradi tu asiseme uongo wala kuzusha jambo.

Usiogope!!

JINSI YA KUPIKA KATLESI


MAHITAJI
  • Viazi ulaya
  • Nyama ya kusagwa
  • Kitunguu swaumu
  • Kitunguu maji
  • Hoho
  • Karoti
  • Mafuta ya kupikia
  • Mayai
  • Pilipili (ukitaka)
MAANDALIZI
  • Menya viazi
  • Vioshe na maji safi
  • Menya na twanga kitunguu swaumu
  • Katakata viungo vipande vidogo vidogo
  • Pasua majai weka kwenye chombo kisafi kisha koroga na chumvi kwa mbali
MAPISHI
  • Chemcha viazi viive
  • Twanga au ponda ponda vilainike
  • Chemsha nyama na chumvi kwa mbali
  • Ikiishaiva weka kitunguu swaumu, kitunguu maji, hoho, karoti na pilipili ukitaka
  • Changanya viungo vyako kwa pamoja vichanganyike vizuri (hakikisha hakuna maji bali mvuke)
  • Weka viazi ulivyoisha viponda
  • Changanya vyote kwa pamoja
  • Chukua kidogo kidogo mkononi
  • Finyanga kwa urefu
zikiwa tayari kwa kukaangwa
  • Tosa kwenye mayai
  • Kaanga kwenye mafuta ya moto
zimeiva, tayari kwa kuliwa
Karibu mezani...




Wednesday, June 22, 2016

JINSI YA KUPIKA TAMBI ZA KUKAANGWA NA MAINI ROSTI



MAHITAJI
  • Maini
  • Tambi
  • Viazi ulaya
  • Nyanya
  • Kitunguu
  • Karoti
  • Hoho
  • Ndimu
  • Kitunguu swaumu
  • Chumvi
  • Mafuta ya kupikia
  • Sukari
  • Iriki
  • Maji safi
MAANDALIZI
  • Kata maini kwa shepu unayotaka
  • Menya viazi kisha kata kata shepu ya maboksi
  • Osha maini na viazi kwa maji safi
  • Katakata viungo vya kupikia (nyanya, kitunguu, hoho na karoti)
  • Menya vitunguu swaumu kisha twangaa vilainike
  • Menya kisha twanga iriki kama punje tano au sita


JINSI YA KUPIKA
*Maini
  • Chemsha maini kidogo kwa maji uliyooshea
  • Weka chumvi na ndimu kidogo kuleta ladha
  • Maji yakiisha kaukia unaweka pembeni kwenye chombo kingine
  • Weka mafuta kiasi ya kupikia
  • Mafuta yakishachemka unaweka kitunguu mpaka kiwe na rangi ya kahawia
  • Weka nyanya
  • Kaanga kaanga nyanya mpaka ziwe rojorojo
  • Weka viazi kisha geuza geuza
  • Weka kitunguu swaumu 
  • Weka maini uliyoyachemsha


  • Koroga koroga mpaka uone maini yanataka kushikana
  • Weka maji kipimo ukitakacho (ila kwa rosti, weka maji kidogo tu kama nusu kikombe cha chai)
  • Vikiishachemka, unaweka karoti na hoho mwishoni
  • Funika vichemke
  • Baada ya muda kidogo unageuza kisha angalia kama chumvi iko sawa (kama bado unaongeza kidogo kabla ya kuipua)
  • Maini yatakuwa tayari kwa kuliwa
*Tambi
  • Chemsha maji yatokote
  • Weka mafuta  kwenye sufuria motoni
  • Yakiishapata moto, vunja vunja tambi kisha ziweke kwenye mafuta
  • Rusha rusha sufuria kuzigeuza mpaka zibadilike rangi kuwa kahawia (brown)
Tambi baada ya kukaangwa (hazijawekwa maji)
  • Weka maji ya moto yafikie juu kidogo ya tambi zinapoishia kwenye sufuria
  • Weka sukari kidogo na iriki uliyoisha itwanga
  • Funika vichemke
  • Angalia angalia kama zimeiva
  • Maji yakikaribia kuisha unatoa sufuria motoni.





Chakula tayari...
Maji mengi huleta mchuzi
Tambi baada ya kuiva



Rosti (haina mchuzi)
Enjoy!!

Monday, June 20, 2016

Courage isn't having the strength to go on, it is going on when you don't have strength...



Napoleon ndiye aliyesema maneno haya " Ujasiri sio kuwa na nguvu za kusonga mbele ila ni kusonga mbele bila ya kuwa na  nguvu".

Binadamu tunakumbwa na changamoto nyingi sana. Wakati mwingine tunapata shida zinazofururiza mpaka tunajiuliza kama Mungu yupo; tukidhani kumetelekezwa njiani. Napoleon anatukumbusha kuwa na nguvu hasa pale tunapokata tamaa kabisa, kwa kufanya hivyo tutakuwa jasiri. Ewe ndugu, usikate tamaa leo. Onyesha ujasiri wako kwa kusonga mbele hata kama unahisi kuelemewa na mizigo ya dunia. Onyesha ujasiri wako hata kama rafiki zako wote wamekukimbia. Onyesha ujasiri kwa kujikongoja bila kuwa na nguvu kwani ni kwa kufanya hivyo, nguvu zitajitengeneza ndani yako na utafanya mambo makubwa mpaka ujishangae. Kuwa jasiri leo...

JINSI YA KUPIKA VIAZI MBATATA, NYAMA YA KUSAGWA NA UJI WA MUHOGO

MAHITAJI
  • Viazi mbatata (viazi ulaya)
  • Nyama ya kusagwa
  • Unga wa muhogo
  • Nyanya
  • Vitunguu
  • Pili pili hoho
  • Karoti
  • Mafuta ya kupikia
  • Maji safi
  • Chumvi
  • Ndimu
  • Pili pili mtama 
  • Ukwaju

MAANDALIZI



  • Menya viazi
  • Kata size unayotaka ama viache vikiwa vizima
  • Vioshe vizuri kwa maji safi
  • Andaa nyanya, vitunguu, hoho na karoti
  • Saga nyama (kama ulinunua ambayo haijasagwa)
  • Kamua ndimu kwenye chombo kidogo
  • Pekecha ukwaju kama unavyotengeneza juisi yake kisha chuja

JINSI YA KUPIKA
*Viazi vya nyama




  • Washa jiko lako
  • Injika sufuria la kupikia jikoni
  • Weka mafuta kwenye sufuria la kupikia
  • Mafuta yakichemka mwaga vitunguu na geuza viive
  • Weka ziazi mbatata kwenye mchanganyiko wako
  • Koroga kwa muda wa dakika kama kumi hivi, mpaka viungulie
  • Tia nyanya na funika ichemke haraka
  • Baada ya dakika moja, funua na geuza
  • Weka nyama ikiwa bado mbichi
  • Nyunyiza mchuzi wa ndimu uliyoisha kamua ili kutoa harufu ya shombo ya ubichi wa nyama
  • Geuza geuza mchanganyiko wako uchanganyike vizuri
  • Acha vichemke kwa dakika kama tano kisha geuza tena
  • Weka hoho na karoti kwa pamoja kisha funika
  • Baada ya dakika tano (kwa moto mdogo usiounguza), funua na koroga vichanganyike vizuri
  • Epua


  • *Uji
    • Bandika maji
    • Acha yachemke yawe vuguvugu
    • Koroga unga kiasi kwenye chombo chenye maji (kama unavyokoroga ugali)
    • Mwaga mchanganyiko ndani ya maji yanayochemka jikoni
    • Acha vichemke kama unavyopika ugali
    • Vikiisha kuchemka, weka ukwaju kidogo kuleta ladha (ikizidi inakuwa chachu)
    • Weka sukari iivie (pima kulingana na uji uliopika
    • Malizia kwa kuweka pilipili mtama kidogo



    Mlo mwema...

    Thursday, June 16, 2016

    Fanya kazi kwa bidii, kuwa na furaha, na tengeneza historia


    Anaitwa Jeff, anasema fanya kazi kwa bidii...lakini si kazi tu, furahi pia na anamalizia kwa kusema tengeneza historia.
    Toka uzaliwe, ni nini umefanya kutengeneza historia? Umefikiria ni nini utaacha kama kumbukumbu ukifa leo?!? Watu wengi wanaaga dunia lakini wachache wanakumbukwa na ulimwengu huku wengine wakikumbukwa na familia zao tu. Kufanya kazi ni wajibu wa kila mtu lakini hakikisha unafurahia kazi uifanyayo ili iwasaidie wengi zaidi ya wewe pekee (oneself). Kwa kufanya hivyo utajenga ukuta imara kati yako na wanaokuzunguka na pengine zaidi za hapo kwa kuujumlisha ulimwengu. TENGENEZA HISTORIA SASA....

    Wednesday, June 15, 2016

    Maisha ya baadaye mali ya yule anayejiandaa leo.

    The Future belongs to those who prepare for it......

    Haya ni maneno ya mwanahistoria mmoja anayefahamika kwa jina la Malcom X.


    Ndugu, ukitaka maisha mazuri ya baadaye sharti ujiandae leo hii. Anza leo, usingoje kesho usiyokuwa na uhakika nayo. Watu wengi hupenda kusubiria kupata mtaji kamili ndipo waanze biashara. wengine husubiri wapate mtoto ndipo wajifunze kulea. wengine wanasubiri mitihani ikaribie ndipo waanze kusoma, wengine wanasubiri shida ndipo wamkumbuke Mungu, wengine hutaka kupunguza miili yao kwa afya njema lakini wanasema "nitaanza kesho au mwezi ujao au tarehe moja (nayo haifiki)". Tusiwe watu wa kusubiri....tuanze sasa. Chochote ulichonacho kiwe kingi au kidogo, anza nacho. UKITAKA MAZURI YA BAADAYE SHARTI UJIANDAE MAPEMA.

    J. A. Y

    Ninajijali, wewe je?

    Tuesday, June 14, 2016

    JINSI YA KUPIKA FUTARI YA MIHOGO NA SAMAKI


    MAHITAJI:
    • Mihogo
    • Nazi
    • Chumvi
    • Samaki
    • Limao/ndimu
    • Mafuta

    *Pilipili manga
    *Kitunguu swaumu
    *Tangawizi

    JINSI YA KUPIKA:
    • Mihogo

    Menya mihogo
    Kata kata vipande vidogo vidogo
    Bandika jikoni
    Acha kwenye moto kwa dakika kumi kama unatumia gesi
    Andaa nazi
    Mimina nazi kwenye mihogo ikiwa bado inachemka
    Tia chumvi kidogo
    Acha vitokote kwa dakika kumi nyingine ili nazi ichemke
    Bonyeza kwa mwiko uone kama imelainika 
    Kama imelainika epua, kama bado ongeza maji kidogo ili iive

    • Samaki

    Andaa samaki wako kwa kuwaparua na kuwaosha vizuri
    Wakate msitari kila upande
    Pakaa chumvi na limao/ndimu
    Pakaa viungo vingine kama pilipili manga, swaumu na tangawizi (ukipenda)
    Weka mafuta kwenye kikaangio
    Injika mafuta kwenye moto yachemke
    Kaanga samaki mpaka wawe na rangi ya kahawia
    Epua

    Waweza kuipamba sahani uliyopakulia chakula chako kwa kachumbari na limao/ndimu kwa ajili ya kuongeza ladha zaidi wakati wa kula.

    Nakutakia mlo mwema....