Wednesday, June 29, 2016

Usilie sababu kimeisha, tabasamu sababu kilitokea.



Dr Seuss ndiye aliyesema maneno hayo, nami nakazia tu hapo. Tumeumbwa na watu wanaotuzunguka tuishi pamoja tukisaidiana kwa  mambo mbalimbali. Katika kushirikiana katika kazi za kibinaadamu hutokea mengi kama vile kupata wenza na pengine kufika mbali nao kwa kuanzisha familia. 
Maisha ni matamu na yenye furaha tunapozungukwa na watu wenye furaha pia. Wao hutusaidia kujenga amani ndani yetu LAKINI, wanapoondoka sisi huumia sana kwani tunakosa ile furaha tuliyokuwa nayo japo kwa muda tu. 
Tunapofiwa ama kuondokewa na wapendwa wetu kwa sababu za kidunia mfano kusafiri, kuachana, kubadili mitazamo n.k, tunaumia kwani nasi ni binaadamu. Lakini kumbe hatupaswi kulia na kusononeka sababu kila kitu kina sababu. Naye Dr Seuss anatukumbusha hayo kwa kusema tutabasamu kwani walau tulikuwa nao, kutaishi na kufurahi pamoja.

Kuwa na mwanzo mpya. Jipe moyo upate amani kwa afya ya moyo wako. Tabasamu! Tabasamu! Tabasamu!

J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Monday, June 27, 2016

CABBAGE (KABEJI)



Kuna cabbage ya rangi ya kijani na ya damu ya mzee (maroon) ila inaitwa tu nyekundu
Leo tutaangalia faida za cabbage katika miili yetu. Kwanini tuile na inatufaidisha nini?

Mboga hii inatuhusu sana kama wanadamu. Ziangalie faida zifuatazo zitokanazo na ulaji wa kabeji:
  • Ziko za rangi tatu tofauti, kijani, nyeupe na nyekundu. Unanafasi kubwa ya kuchagua ni ya rangi ipi ule. Ya kijani ikikuchosha unakula nyekundu.
  • Haina kiwango kikubwa cha mafuta hivyo hainenepeshi ukiila sana; badala yake inakusaidia kuujenga mwili vizuri sababu ya nyuzi nyuzi zitokanazo na mboga hiyo.
  • Husaidia wajawazito katika kumlinda mtoto awapo tumboni pamoja na kukuza tumbo la mimba bila kuongeza mafuta. Hapo hapo ni chanzo cha folate ambacho ni kipengele kimoja wapo cha DNA (deoxyribonucleic acid-husaidia ugunduzi wa kirithi kwa mwanadamu katika seli (cell) karibuni zote katika mwili); hivyo, huleta uhusiano mzuri wa mama na mtoto.
  • Huipa mifupa na mwili nguvu sababu ya Vitamin C inayoupa mwili nguvu kujiepusha na magonjwa kwa haraka na Vitamin K ambazo husaidia katika kuleta nguvu kwenye mifupa hivyo kusababisha isilegee ama kujikunja. 
  • Inamadini kama Calcium, Potasium, Phosphorus, Manganese, Iron na Magnesium ambayo husaidia kiwango cha moyo na presha ya damu. 
  • Madini ya chuma (Iron) ni muhimu sana sababu huleta chembe chembe nyekundu za damu ambazo husaidia wakina mama wajawazito kutokuwa na upungufu wa damu. 
  • Ni mboga ya msimu. Haivunwi mara kwa mara hivyo inapopatikana ile kwa wingi kabla hujaikosa isipokuwepo.

  • Kabeji nyekundu husaidia kuzuia kansa kwa kuachisha ukuaji/uzalishaji wa seli za cancer.
Kikombe kimoja cha kabeji nyekundu kina 33% ya Vitamin A ambazo tunapaswa kula kila siku.
EMBU ANDAA KABEJI YAKO SASA...

*Waweza iunga kwa kitunguu pekee.
*Waweza ikaanga na chumvi.
*Waweza iunga na kitunguu na nyanya.
*Waweza ipika kwa viungo vyote yaani nyanya, kitunguu, karoti, hoho, pilipili na mazaga mengine unayoyafahamu.
*Waweza ipika kwa karanga au nazi.
*Wengine hupendelea kuiweka kwenye kachumbari. 
*Wale wa diet, inachemswa bila mafuta wala chumvi...kazi kwako!!

J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Friday, June 24, 2016

SHAMBA


Haihitaji kuwa na eneo kubwa ili uanzishe bustani. Bustani ya mboga mboga nyumbani kwako sio tu itakuletea muonekano mzuri wa nyumba yako kwa nje lakini pia, itakusaidia kupata chochote kiendacho kinywani.

Ugumu wa maisha na kupanda na kushuka kwa bei ya vyakula hufanya watu wale mlo mmoja. Lakini unapopata hela ya mboga ukaitunza sababu mboga ziko shambani, basi hiyo akiba unaweza inunulia nyama. Hahah! Hudumia familia yako basi.

Anzisha shamba la matunda na mboga mboga. Anzisha shamba dogo la kile uwezacho. Waweza kuwa na la mchicha au  matembele tu kwa kuanzia. Tunza hela kwa kununua mboga kila siku ambazo unaweza zipata kwako. ZAIDI, utakuwa unapata klilicho salama zaidi


J.A.Y

Ninajijali, wewe je?

Thursday, June 23, 2016

LAKINI SOTE TUNAOGOPA KUSEMA VILIVYO NA THAMANI KUSEMWA...


Hofu ya mwanadamu hutofautiana kwa ukuu. Lakini sote huogopa kwa namna fulani. Hata mwenye nguvu huhofia wenzao wenye.

Tuogope yote lakini tusiogope kusema ukweli inapobidi, na si ukweli tu ila kuzungumza kwa ujumla.

Wapo wenye mawazo mazuri sana ambayo yasipokaliwa kimya yanaweza kuleta athari kubwa tu kwa mtu mmoja au jamii nzima.
Yamkini ukambadilisha mtu / watu, ukaokoa maisha ya mtu / watu, ukapata msaada ulioukusudia au kuutamani kwa muda mrefu, ukatambulika katika familia, ukoo, eneo, nchi, bara au dunia kwa kusema kwako.

Usisite, usikate tamaa, usiogope kusema sababu yule ni mtu mzima, yule ni mkali, yule ni mpole sana, yule haeleweki, yule simuamini. Usihisi labda hivi, labda vile. Sema usikike hata kama utamkwaza, hata kama utamuudhi, hata kama atakujibu vibaya, atakukaripia, atakutukana ama atakukalia kimya. Katika yote, hakika kuna ambalo litamgusa na kumbadilisha japo kidogo.

Kama ni cha thamani kiseme...kitaleta mabadiliko!! Kiseme, moyo wako uridhike pia!!

Katika sehemu ya tatu, kifungu cha 18 cha Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, tunaona kuwa kila mwanadamu anauhuru wa kuongea / kuzungumza. Kumbe basi, ni wajibu wa kila mmoja kuzungumza kile anachoona ni sahihi, ilimradi tu asiseme uongo wala kuzusha jambo.

Usiogope!!