Monday, April 4, 2016

KIFUA KIKUU

JE, UNAUFAHAMU UGONJWA WA KIFUA KIKUU?
Naibu meneja wa mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma, Dr. Liberate Mleoh, anaelezea zaidi juu ya ugonjwa huu.










Kifua kikuu (Tuberculosis-TB) kimegawanyika katika aina mbili; cha ndani ya mapafu na nje ya mapafu. Kifua kikuu cha ndani ya mapafu ndicho kinachojulikana zaidi na kinasumbua zaidi. Sasa je, kifua kikuu hiki kikoje?

Ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea ambavyo vinamkuta mtu na kuharibu mapafu. Ugonjwa huu unaenea kwa njia ya hewa ambapo mtu mwenye vimelea hivyo anapokohoa ama kupiga chafya anaweza kumuambukiza mtu wa karibu naye ambaye hana vimelea hivyo. 

Tanzania ni nchi ya ishirini na mbili inayoongoza kuwa na tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu duniani lakini ni ya sita kwa Africa. Katika utafiti uliofanyika 2012 ili kujua ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu Tanzania, imegundulika kuwa, katika watu laki moja kuna wagonjwa wasiopungua 528 na uwezo wa watanzania kugundua wana kifua kikuu ni 36%.

Ni jukumu la kila mmoja wetu basi kufuatilia kwa kupima mara kwa mara kama tatizo hilo lipo au la. Kama lipo basi matibabu yaanze mara moja ili kuepuka kuusambaza zaidi. Dr. Mleoh amesema mtu akitumia dawa kwa wiki mbili mpaka mwezi mmoja anapunguza hatari ya kumuambukiza asiye na vimelea vya ugonjwa. Sasa basi, kila mtu achukue hatua kwa afya yake.

Kinachosababisha kifua kikuu ni mdudu (Mycobacterium Tuberculosis). Mdudu huyu anangozi ngumu kwa jina la utani wanasema "amevaa koti" hivyo inakuwa ngumu kumtibu kwa dawa ya kawaida. Dawa zinazotumika ni za mseto yaani ni zaidi ya moja. Mtaalamu anasema zinatumika dawa nne ndani ya kileo kimoja na inatumika kwa muda mrefu ambapo ni miezi sita mpaka nane kulingana na ukali wa tatizo; kama ni sugu basi dawa zitatumika kwa miezi isiyopungua ishirini.

 Ni zipi dalili za ugonjwa wa kifua kikuu?

1. Kukohoa mfururizo kwa wiki zisizopungua mbili; kikohozi cha kawaida ama kilichochanganyikana na damu.
2.Kutokwa jasho lisilo la kawaida hasa kwa wakati wa usiku.
3. Kukosa hamu ya kula.
4. Kupungua uzito.
5. Homa za jioni.
6. Uchovu.

Ugonjwa huu unatesa sana lakini unatibika. Pima afya yako sasa upate kujua kama uko salama au la. Kama uko salama basi jiepushe na uvutaji wa hewa kutoka kwa yeyote anayehohoa kwani huwezi jua yupi anavimelea vichanga. Lakini pia, kama wewe ni mmoja wa wagonjwa yaani umepima ukagundulika na vimelea vya tuberculosis mycobacterium basi jaribu kumkinga mwenzio kwa kuziba mdomo wakati unakohoa pamoja na kukohoa mbali naye. Tumia dawa ipasavyo  ili kuviua vimelea vyote mwilini kwa afya bora.
Tatizo la watanzania wengi bado hawajaufahamu vizuri ugonjwa huu. Wewe uliyesoma mueleweshe na mwenzako. Kwa pamoja tutaweza kuutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu na kulinda miili yetu isidhoofike. 
Kuwa imara, jali afya yako.















No comments:

Post a Comment