Friday, April 22, 2016

MoYo


Je, unaufahamu kuwa kila mwanadamu anapumua kwa msaada wa moyo? Na je, unafahamu kuwa moyo huo huo unaweza kumfanya mtu kuwa na furaha ama huzuni? 

Hii ni alama ambayo wengi huitumia kuashiria moyo na moyo huo basi unatumika kama ishara ya upendo. 
Moyo ni pampu inayosukuma damu kupitia mishipa ya damu. Kupitia mishipa hiyo damu husambazwa mwili mzima ili kukupatia hewa safi (oxygen). Tukiachana na maswala ya kibaiolojia, moyo unakazi ya kupenda.

Basi tuone upendo huo unaathiri vipi moyo na wewe kama binadamu unaukosea vipi moyo wako ama moyo wa mwingine. Jijali, mjali na mwenzio ili kuufurahisha moyo kwa afya zaidi. 



Huu ni moyo wa binadamu. 
Unapokuwa umezungukwa na watu wakupendao haijalishi ni upendo wa aina gani, moyo huwa na nguvu na hufanya kazi yake vizuri. Kila mmoja anapenda kupendwa, hata wababe huwa na wafuasi wao hata kama hawana upendo wa dhati.
Moyo wenye furaha. 
Moyo wenye nguvu

Moyo wenye furaha huimba ndani yetu pale tunapoongeza marafiki wapya. Moyo wenye furaha huupoza mwili tusikiapo baridi yaani tuwapo wapweke, kwa kukumbuka mema mengi yaliyopita. Inawezekana kabisa kwa wewe kujichangamsha bila kusubiri kuchangamshwa.

Moyo imara ni moyo wenye nguvu kwani unaweza kupigana na majaribu yote yanayotukumba katika maisha. Sisi sote tunapaswa kuwa na moyo wenye nguvu kwani pia ni rahisi kupingana na magonjwa tukianza na ugonjwa wa 'moyo' wenyewe.

Upendo wa nguvu
Upendo wa mahusiano ya kimapenzi ni upendo unaoleta hisia za kipekee. Kila mmoja anaweza kuuelezea ajuavyo yeye. LAKINI, maumivu ya kuachana kwa wapenzi hao yanaweza kuwa yanafanana kwani yote huumiza moyo.

Upendo unaolega lega
Afya ya mtu ni ya thamani, ni vema kutumia nafasi unayopata kwa mpenzi wako kumuonesha upendo na kupata upendo kutoka kwake. Kama unadhani hujaamua bado kujiingiza kwenye mahusiano, basi tafakari kabla ya kuchukua hatua. Ni vema kujiamini kwa ulifanyalo kuepukana na maumivu ya moyo. Kipindi tu unapojihusisha na mahusiano ya kimapenzi, fahamu kuwa unajifunga. 

Moyo uliofungwa kwa upendaye,
usiufungulie kwa wengine. 
Angalizo: Ili kuulinda moyo (wako/mwemzako) na maumivu zingatia haya:-
  • usiruhusu mtu kukuzoea haraka
  • usitoe siri zako 
  • usiseme udhaifu wako 
  • usijihakikishie mahusiano marefu (ingawa inapaswa kuwa hivyo)
  • usimchagulie mtu mpenzi
  • usimlazimishe mtu kukupenda
  • usijilazimishe kumpenda mtu
  • usimtumie mtu kama njia ya kumsahau aliyekuumiza
  • usiogope kumuambia unampenda (kama ndio mmeonana) bila kujali wewe ni ME au KE.
  • usipoteze muda mwingi kujifikiria juu ya jibu la kutoa 
  • usianzishe mahisiano mengine wakati uliyonayo sasa hayajaisha
  • usiwe mkimya sana wala mchangamfu kupita kiasi (utaboa)
  • usisubiri kutafutwa, anza pia (usitegee)
  • usingoje kusaidiwa, saidia pia (ushirikiano)
  • usiwe mkali sana ama mbabe kwa mwenzio
  • mkumbatie kwa muda mrefu kila upatapo nafasi (kumbato husaidia kuondoa huzuni kwa kiasi fulani lakini pia huzidisha ukaribu)
  • mpatie zawadi ndogo ndogo (mfanye atabasamu)
  • mchekeshe kwa vistori na michejo
  • muombe msamaha hata kama amekosa yeye
  • mwambie unampenda mara kwa mara
  • usijaribu mahusiano na mtu mwenye mahusiano
Ukipata mwenzako mshikilie sawa sawa
Ni bora kuumia kidole kitapona au kuvunjika kidole vingine vitafanya kazi lakini sio kuumia moyo sababu maumivu yake yaweza kuchukua miaka kuisha na kuvunjika kwa moyo ni ngumu kuutengeneza ukafanya kazi sawia.
Moyo usioweza
kufanya maamuzi
sahihi
Moyo ulionyong'onyea
na kudhoofika
Moyo
uliochanganyikiwa.
Hapa ndipo tunaposhauriwa kuwa na imani kwa kumuomba Mungu kwani yeye ndiye aliyekupa maisha. Jijali kwa kuepukana na athari hizo lakini pia, kama ikitokea ushaumizwa basi jitahidi kujishughulisha sana ili kupunguza mawazo. Kaa na watu watakupa mawazo tofauti usikae mwenyewe ukiwa mpweke kuepukana na mawazo potofu. Kemea roho ndani yako inayokusukuma kukata tamaa, kuchukia ama kujiua. Sali sana ukisikia hivyo kwa afya ya Roho na moyo pia.

Maumivu makali ya moyo 
Usiuzeeshe moyo wako kwa mambo usiyoyaweza. Usiukondeshe kwa kuupa mambo mengi usiyoweza kuyafuatilia na kuyafanya kwa ufanisi, usiufanye ukaelemewa. Ujali moyo wako kwa kujipenda na kuwa makini. Lakini kikubwa, usiutegemee moyo pekee katika mapenzi, shirikisha akili yako. Ni kwa kufanya hivyo, moyo utabaki kupenda tu huku mengine yakifanywa kwa utashi uliobarikiwa nao.

Thursday, April 21, 2016

Urefu wa kupindukia

Wewe ni mrefu? Ni mara ngapi umekutana na watu warefu? Ni nini kinafanya mtu awe mrefu? Fuatilia.....

Wanabiolojia wa molekuli (molecular biologists) wanaeleza kuwa tofauti ya urefu wa mtu na mtu kwa asilimia 60 mpaka 80 unatokana na maumbile huku asilimia 20 mpaka 40 unatokana na sababu za mazingira hasa lishe.  Urefu wa maumbile sana sana ni ule unaorithiwa hasa kutoka kwa mwanafamilia ama ndugu wa karibu.

Kila mmoja anahomoni za ukuaji (somatotropin) ambazo zinamsababisha kurefuka haraka ama taratibu. Utofauti huu ndio unaoleta utofauti katika urefu wa mtu na mtu.
Hizi homoni zina protini 191 zenye amino acid na uzito wa daltoni 22,124; na huzalishwa kwenye glandi iitwayo pituitary ambayo husambaza homini hizo mwilini kwa ajili ya ukuaji mara baada ya uzalishaji wake.

Wengi wetu tutakumbuka msemo wa wazazi kwa watoto wao wa "lala ukue" kama kumuhamasisha aende kulala hasa wakati wa mchana ambapo watoto wengi hupenda kuutumia kucheza. Inawezekana baadhi wa wazazi wanautumia kama mazoea lakini msemo huo unaukweli ndani yake.

Usambazaji wa homoni huchukua muda wa masaa matatu hadi matano lakini mtu hurefuka haraka ndani ya lisaa limoja tu akiwa amelala usingizi mzito. Hivyo ukuaji kutokea mara baada ya usambazaji wa homoni zinazohusika na ukuaji. Zikisambaa haraka na kwa wingi ndivyo mtu akuavyo mrefu zaidi kwa kipindi kifupi tu.

Homoni hizi hufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa watoto na vijana ambao wako katika kipindi cha ukuaji, na si kwa mtu mzima. Wazazi tuwashauri watoto wetu kupata usingizi wa kutosha ili kumsaidia kukua haraka.

Yamkini hawa ni wapenzi, pamoja na kuwepo kwa tofauti zao kiurefu bado wanaonekana kupendana. (picha kushoto)

Hawa nao ni marafiki, wao huchweza pamoja mpira wa kikapu. Wanaonekana kuwa wenye furaha sana ukiweka kando ukweli kuwa wamepishana sana urefu. (picha chini kulia)


Hivyo, kama wewe ni mrefu kuzidi wenzako usijione wa tofauti sana, kaa nao, cheza nao, furahi pamoja nao na wala usijitenge kwani furaha yako ni furaha ya jamii nzima.
Na kama wewe si mrefu usijishangae pia na wala usimtenge aliye mrefu zaidi yako.

Kinachofanya mtu awe mkubwa zaidi au mdogo zaidi ni sehemu ya mbele ya glandi ya pituitary iitwayo 'anterior pituitary'. Ikifanya kazi kupita kiwango humfanya mtu kuwa mrefu mno yaani 'giant' na vile vile inapofanya kazi chini ya kiwango basi mtu huwa mfupi zaidi yaani 'dwarf'.

Ewe kijana, unataka kuwa mrefu? Nawe mzazi, unataka mwanao arefuke vizuri? basi kama uko kwenye umri wa ukuaji bado unayo nafasi. Epukana na vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi (junk food). Pata lishe iliyobora kuisaidia glandi inayohusika na homoni za ukuaji kufanya kazi sahihi katika mwili wako. Hakikisha unapata usingizi wa kutosha ili kurahishisha somatotropin (homoni za ukuaji) kufanya mzunguko vizuri katika mfumo wake.


Kunywa maziwa ili upate calcium itakayokuimarishia mifupa yako. Urefu ukiambatana na mifupa legevu unaweza kupata matege lakini ukipata calcium basi unakuwa imara muda wote. Kula vyakula vyenye amino acid mfano samaki, mayai, mboga mboga kama mabilinganya na matunda kama karoti matikiti na maepo.

Monday, April 18, 2016

Maziwa mtindi


Maziwa mtindi yanavirutubisho vingi sana vinavyopendkezwa kuwa na faida nyingi katika mwili wa binadamu. 
Ni lini mara yako ya mwisho kupata maziwa mtindi? Pata kama chakula ama baada ya chakula ama kabla ya chakula, yatakusaidia. Soma faida zake hapa.

Kabla ya kuzifahamu faida ya maziwa mtindi kwanza tuone virutubisho vichache vinavyopatikana ndani yake. Mtindi una calcium, phosphous, riboflavin (vitamin B2), iodine, vitamin B12. panantothenic acid (vitamin B5) zinc, potassium pamoja na molybdenum. Mbali na virutubisho hivyo, maziwa mtindi pia yana wadudu ambao ni "bakteria hai" wenye umuhimu mwilini kiafya. 

Kuna homoni (cortisol) sehemu ya katikati ya tumbo na kiuno ambayo inakazi ya kuamuru ubongo kuongeza mafuta chini ya tumbo hivyo kusababisha kitambi. 

Maziwa mtindi husaidia kupunguza ama kuondoa kabisa kitambi kwa asilimia 82; kwa msaada wa madini ya calcium yaliko kwenye mtindi ambayo hupunguza homoni inayoamuru mafuta kwenda chini ya kiuno.

Ni vema kunywa kutumia maziwa mtindi mara moja moja hasa wakati wa jioni unapokuwa umepumzika yaani baada ya shughuli zako.
Pata mtindi ukiambatanisha na maji mengi ili kurahisisha mfumo wa upatikanaji wa maji mwilini. Mtindi huufanya mwili kuwa na maji muda wote yaani usiwe mkavu.
aida zingine ni pamoja na: 


  • Kurefusha maisha kwani yanauwezo wa kupambana na magonjwa.
  • Ni kinga kwa kina mama kwani inakinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza ukeni (vaginal infections).
  • Ni kinga ya mwili kwani inapambana na magonjwa kama saratani mfano saratani ya utumbo.
  • Kuondoa lehemu (cholesterol) mbaya mwilini hilo kumuepusha mtu na tatizo la shinikizo la damu.
  • Kupunguza uzito kwa asilimia 22 kwani yanapunguza mafuta mwilini.
  • Yanasaidia kukupa seli za misuli yako kupitia virutubisho vya protini.
  • Yanasaidia kuupa mwili nguvu kupitia virutubisho vya wanga.
Chonde: Usitumie maziwa ya mtindi yatokanayo  na maziwa ya unga kwani utakosa ule uchachu na bakteria hai wenye umuhimu mwilini, hivyo kukosa virutubisho mwilini. 

Unaweza pata maziwa mtindi kama mboga ukala na ugali, unaweza kuyanywa yenyewe kama chakula, unaweza kuyanywa na kitafunwa kama biskuti, mkate au maandazi.


Wengi wetu hupenda kupunguza miili kwa mazoezi lakini jambo kubwa tunalosahau ni lishe bora na / mlo kamili. Ukifanya mazoezi ukaendelea kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi, hutakuwa umepunguza tatizo. Fanya mazoezi kisha pata maziwa mtindi ujionee tofauti. 

Monday, April 4, 2016

KIFUA KIKUU

JE, UNAUFAHAMU UGONJWA WA KIFUA KIKUU?
Naibu meneja wa mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma, Dr. Liberate Mleoh, anaelezea zaidi juu ya ugonjwa huu.










Kifua kikuu (Tuberculosis-TB) kimegawanyika katika aina mbili; cha ndani ya mapafu na nje ya mapafu. Kifua kikuu cha ndani ya mapafu ndicho kinachojulikana zaidi na kinasumbua zaidi. Sasa je, kifua kikuu hiki kikoje?

Ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea ambavyo vinamkuta mtu na kuharibu mapafu. Ugonjwa huu unaenea kwa njia ya hewa ambapo mtu mwenye vimelea hivyo anapokohoa ama kupiga chafya anaweza kumuambukiza mtu wa karibu naye ambaye hana vimelea hivyo. 

Tanzania ni nchi ya ishirini na mbili inayoongoza kuwa na tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu duniani lakini ni ya sita kwa Africa. Katika utafiti uliofanyika 2012 ili kujua ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu Tanzania, imegundulika kuwa, katika watu laki moja kuna wagonjwa wasiopungua 528 na uwezo wa watanzania kugundua wana kifua kikuu ni 36%.

Ni jukumu la kila mmoja wetu basi kufuatilia kwa kupima mara kwa mara kama tatizo hilo lipo au la. Kama lipo basi matibabu yaanze mara moja ili kuepuka kuusambaza zaidi. Dr. Mleoh amesema mtu akitumia dawa kwa wiki mbili mpaka mwezi mmoja anapunguza hatari ya kumuambukiza asiye na vimelea vya ugonjwa. Sasa basi, kila mtu achukue hatua kwa afya yake.

Kinachosababisha kifua kikuu ni mdudu (Mycobacterium Tuberculosis). Mdudu huyu anangozi ngumu kwa jina la utani wanasema "amevaa koti" hivyo inakuwa ngumu kumtibu kwa dawa ya kawaida. Dawa zinazotumika ni za mseto yaani ni zaidi ya moja. Mtaalamu anasema zinatumika dawa nne ndani ya kileo kimoja na inatumika kwa muda mrefu ambapo ni miezi sita mpaka nane kulingana na ukali wa tatizo; kama ni sugu basi dawa zitatumika kwa miezi isiyopungua ishirini.

 Ni zipi dalili za ugonjwa wa kifua kikuu?

1. Kukohoa mfururizo kwa wiki zisizopungua mbili; kikohozi cha kawaida ama kilichochanganyikana na damu.
2.Kutokwa jasho lisilo la kawaida hasa kwa wakati wa usiku.
3. Kukosa hamu ya kula.
4. Kupungua uzito.
5. Homa za jioni.
6. Uchovu.

Ugonjwa huu unatesa sana lakini unatibika. Pima afya yako sasa upate kujua kama uko salama au la. Kama uko salama basi jiepushe na uvutaji wa hewa kutoka kwa yeyote anayehohoa kwani huwezi jua yupi anavimelea vichanga. Lakini pia, kama wewe ni mmoja wa wagonjwa yaani umepima ukagundulika na vimelea vya tuberculosis mycobacterium basi jaribu kumkinga mwenzio kwa kuziba mdomo wakati unakohoa pamoja na kukohoa mbali naye. Tumia dawa ipasavyo  ili kuviua vimelea vyote mwilini kwa afya bora.
Tatizo la watanzania wengi bado hawajaufahamu vizuri ugonjwa huu. Wewe uliyesoma mueleweshe na mwenzako. Kwa pamoja tutaweza kuutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu na kulinda miili yetu isidhoofike. 
Kuwa imara, jali afya yako.